Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa AngaTanzania (TCAA) Bw. Hamza Said Johari
Na. Georgina Misama – MAELEZO
Serikali ya Tanzania inatarajia kupokea Dola Milioni Moja kutoka Serikali ya China kupitia Shirika la Anga Duniani ili Kuboresha baadhi ya miundombinu katika sekta ya anga.
Fedha hizo zitatumika kuendeleza baadhi ya maboresho ambayo tayari Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeshaanza kuyafanyia kazi.
Akiongea katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoratibiwa kwa pamoja kati ya Idara ya Habari na TBC na kurushwa kupitia TBC 1, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Hamza Johari amesema kuwa Mamlaka yake imeimarisha usalama katika sekta ya anga ili kuvutia mashirika mengi zaidi ndege kuja tanzania.
“TCAA inafunga rada 4 katika vituo vya Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro na Mbeya ili kuongeza ufanisi na mapato, kuboresha usalama wa anga na kuzuia uwezekano wa anga letu kukasimiwa kwa nchi nyingine yenye uwezo zaidi kiuongozaji ndege” alieleza Bw. Hamza.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu alisema kuwa Mamlaka imefanya kazi ya kuboresha Chuo cha Usafirishaji Tanzania (NIT) ili kupunguza gharama za kuwapeleka Watanzania nje ya nchi kusomea urubani, sambamba na kudhibiti vyuo vyote vinavyotoa elimu katika sekta ya anga kwa kuvipa uthibitisho na vyeti.
Akiongelea swala la sheria zinazoongoza Mamlaka, Bw. Hamza aliwapongeza Wabunge wa Tanzania kwa kusaidia kurekebisha sheria mbalimbali za sekta ya anga ili ziendane na wakati.
Kutokana na maboresho hayo, TCAA imeweza kufaulu ukaguzi wa Kimataifa wa ICAO kwa kupata asilimia 64.7 juu ya viwango vya Kimataifa vya asilimia 60. Nchi ilipokaguliwa Mwaka 2013 ilipata asilimia 37.
Kwa kupata ufaulu kwa asilimia 100, Tanzania itatunukiwa cheti na nishani ya Rais wa ICAO mwishoni mwa Mwaka 2017.
Mamlaka inaipongeza serikali ya Tanzania kwa kulirudisha kwa kasi shirika la ndege Tanzania (ATCL) sambasamba na kuyataka mashirika ya ndege nchini kufuata sheria zinazoongoza sekta ya anga.
“Watoa huduma katika Sekta ya Anga wanapaswa kuwajibika iwapo watumiaji wa huduma hiyo watapata tatizo kwa makosa ya uzembe wa shirika”, alisema Bw. Hamza.
Alieleza kuwa iwapo mtumiaji wa huduma ya usafiri wa anga atapata tatizo la ucheleweshaji wa ndege anatakiwa alipwe dola 6000, upotevu wa mizigo anatakiwa alipwe 1500, kama ni ajali, mtoa huduma anapaswa kulipa dola 120,000 na kuendelea.
Pia Bw. Hamza alifafanua kuwa iwapo mtumiaji wa huduma za usafiri wa anga atapata tatizo kati ya hayo anapaswa kutoa taarifa za kimaandishi kwa Shirika husika, Baraza la watumiaji na kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga.