Na Mwandishi Wetu
JENGO la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII) linalotarajiwa kukamilika Desemba 2018, litafungwa mfumo wa huduma ya viza kwa njia ya mtandao (e-visa) ambao utarahisisha na kuharakisha upatikanaji wake.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhamiaji cha JNIA, Bw. Kaanankira Mbise amemwambia Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano), Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye alipotembelea eneo la uombeaji viza kwa abiria wa kimataifa wanaowasili, kuwa wanatarajia kutumia huduma hiyo ambayo ni rahisi na haraka.
“Tayari mkakati umeanza wa kuanzisha huduma hii ya e-visa hivyo tukifanikiwa utafungwa katika jengo hili jipya, ambapo itasaidia kwa abiria kuipata huduma hiyo kwa haraka kwani itatumia mtandao,” amesema Bw. Mbise.
Hata hivyo, Bw. Mbise amesema kwa sasa wameboresha huduma hiyo kwa wasafiri wanaowasili katika jengo la pili la abiria (JNIA-TBII) ambapo tayari wamepatiwa mashine nne za kisasa zinazosaidia kupunguza msongamano wa abiria wenye kuhitaji huduma hiyo hususan kipindi cha mchana chenye ujio wa ndege nyingi za nje ya nchi.
“Hizi mashine zimeharakisha upatikanaji wa huduma kwani tumeweza kuhudumia abiria wengi kwa wakati mmoja na msongamano umepungua tofauti na awali mashine zilikuwa chache.” amesema Mbise.
Naye Mhe. Mhandisi Nditiye amesema baada ya ziara yake amegundua mashine za viza ni za muda mrefu na zinahudumia abiria mmoja kwa muda mrefu, na tayari ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuwasilisha kwa maandishi mapendekezo yao ya namna ya kuharakisha huduma hiyo ili serikali iyafanyie kazi kwa kusaidia kuondoa kero hiyo.
“Nimegundua kuna baadhi ya mashine za viza zimeongezwa lakini pia zilizopo zimechoka kwani ni za muda mrefu na zinahudumia abiria mmoja kwa muda mrefu na hii inaharibu sifa ya kiwanja chetu kwa wageni wanaokuja hapa nchini,” amesema Mhandisi Nditiye.
Hata hivyo, amesema wanampango wa kuongeza madirisha ya benki yanayolipia viza hizo ili kuharakisha huduma hiyo ambapo sasa ni machache kulinganisha na idadi kubwa ya abiria wanaowasili kwa ndege kubwa zikiwemo za Emirates, Etihad, Oman Air, Qatar, South Africa Air na Ethiopia, ambazo zimekuwa zikipishana kwa muda mfupi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Richard Mayongela amesema tayari wanampango wa kuongeza upana wa eneo hilo la wasafiri wa kimataifa wanaowasili kwa sababu lina msongamano kutokana na ufinyu wake.
“Hili jengo linazaidi ya miaka 30 na ukiangalia abiria waliokuwa wamekadiriwa wakati ule lilikuwa likikidhi mahitaji lakini sasa abiria wameongezeka na eneo limekuwa dogo hivyo tayari tumeanza kwa kuondoa baadhi ya ofisi ili kuongeza upana wake, ninaimani litapunguza msongamano uliopo sasa,” amesema Bw. Mayongela.
Lakini pia Bw. Mayongela amesema sasa wapo katika mazungumzo na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) ili kuangalia namna bora ya kuzipangia muda ndege zinazopishana muda mdogo kwa wakati wa mchana ili ziachiane muda mrefu ambapo kutasaidia kupunguza msongamano.
Awali eneo hilo lilikumbwa na changamoto kubwa ya msongamano wa abiria wanaohitaji huduma ya viza baada ya uchache mashine zinazosimamiwa na Idara ya Uhamiaji zilizokuwepo na kufanya abiria wanaohitaji huduma hiyo kutumia muda mrefu kuipata.