Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TBC Kuhakikisha Usikivu Unafika Nchi Nzima
Nov 18, 2022

Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) limeendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata haki ya kupata habari kwa kufikisha usikivu wa redio zake nchi nzima.

Hayo yameelezwa na  Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa TBC  leo jijini Dar es salaam.

“TBC imekuwa na mikakati ya kuhakikisha kuwa usikivu unafika nchi nzima hususani maeneo ya pembezoni ya nchi yetu, hakikisheni mnajadili mipango na mikakati itakayowezesha usikivu wa redio za TBC kuwafikia wananchi wote”. Ameeleza Naibu Waziri Kundo.

Aidha, ametaja maeneo mengine ambayo TBC inatakiwa kujadili ili kuongeza usikivu kuwa  na watumishi wenye weledi, kuwa na mitambo na vifaa vya kisasa, mazingira bora ya kufanyia kazi, mikakati ya kuongeza mapato ya Shirika, kuandaa vipindi vyenye ubunifu na kuwa na habari zinazovutia wakigusa nyanja mbalimbali na makundi yote katika jamii.

“Ninawapongeza Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wote wa TBC kwa maendeleo makubwa na maboresho mengi yaliyofanyika maeneo ya studio, vipindi vyenye ubunifu na maslahi ya wafanyakazi. TBC ni chombo cha Utangazaji cha Taifa, hakikisheni mnakuwa mbele muda wote katika kuleta furaha kwa Watanzania kupitia vipindi na huduma zote mnazozitoa ili vyombo vingine vya habari viendelee kujifunza kupitia TBC” . Amebainisha Naibu Waziri huyo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kundo amesema kuwa Wizara  itahakikisha kuwa TBC inakuwa na uwezo wa kifedha na rasilimali watu muda wote na kuwa Serikali imeendelea kuipatia TBC fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na matumizi mengineyo.

Fauka ya hayo, Naibu Waziri huyo ameipongeza TBC  kwa ubunifu wa kuwa na Aridhio, Jambo Tanzania Mpya na Taarifa ya Habari ya Kiingereza yenye lengo la kueleza habari kwa mtazamo wa kiafrika, ambapo kupitia taarifa hiyo itasaidia kuifungua nchi kimataifa.

Mipangilio
Marekebisho ya Lugha
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi