Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), imetakiwa kutekeleza miradi wanayoisimamia kwa wakati na kuzingatia weledi ili kuongeza tija na uzalishaji katika Wakala huo.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga wakati akifungua kikao cha siku mbili cha Baraza la wafanyakazi wa Wakala huo, jijini Dodoma.
Agizo la Katibu Mkuu huyo limefuatia baada ya kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya wateja wa Wakala huo amabapo wamesema kuwa Wakala huo umekuwa ukichelewesha miradi, hivyo amewataka kupitia Baraza hilo kujiwekea malengo na mpango mkakati wa kutekeleza miradi hiyo na kuikamilisha kwa wakati.
“Nina uhakiaka suala hili lipo chini ya uwezo wenu endapo mtajipanga vizuri na kufanya kazi kwa mshikamano na weledi huku mkithamini mchango wa kila mmoja wenu katika eneo la kazi, basi mtafanikiwa,” amesema Mwakalinga.
Aidha, ameutaka Wakala huo kujiwekea maazimio yatakayowasilishwa Wizarani ambayo yatajikita katika uboreshaji wa maslahi ya watumishi, ikiwemo kuwajengea uwezo utakaowafanya kutimiza majukumu yao kwa wakati na ufanisi zaidi.
Kuhusu madai ambayo Wakala unadai Taasisi nyingine za umma, Katibu Mkuu Mwakalinga ameutoa hofu Wakala huo kwa kusema kuwa suala hilo halitafumbiwa macho na atahakikisha kuwa madeni yote yanalipwa baada ya kuhakikiwa.
“Wekeni kumbukumbu zenu za madai vizuri ili ziweze kuhakikiwa kabla ya kuwasilishwa kwa wahusika, nami naahidi kufuatilia madeni haya na kuhakikisha kuwa yatalipwa,” amesisitiza Katibu Mkuu.
Ameongeza kuwa Serikali inathamini mchango wa Wakala huo katika kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda ambapo amefafanua kuwa Wizara yake pamoja na Taasisi zilizo chini yake imejiwekea agenda madhubuti ambazo anaamini zikitekelezwa basi Sekta ya Ujenzi nchini itakuwa kwa kasi.
Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daudi Kondoro amemhakikishia Katibu Mkuu huyo kuwa atatekeleza maagizo yote na pia atahakikisha maazimio watakayo jiwekea yanatekelezwa kwa wakati.
Alisema kuwa taratibu za kupandisha watumishi vyeo zinaendelea ambapo tayari watumishi 64 waliokidhi vigezo wamepandishwa vyeo katika madaraja mbalimbali na watumishi 17 wamebadilishwa kada kulingana na taaluma zao.
Kikao hicho kimejumuisha zaidi ya wajumbe 62 ambao baadhi yao ni wakuu wa idara na vitengo, mameneja kutoka mikoa yote, wawakilishi wa wafanya kazi kutoka idara na vitengo pamoja na wawakilishi kutoka vyama vya wafanyakazi vilivyomo ndani ya Wakala.