Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tatizo la Maji Longido Kuwa Historia
Aug 19, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Prisca  Libaga  Maelezo  Arusha

Tatizo la maji katika wilaya ya Longido iliyopo mkoani Arusha linaelekea kuwa historia baada ya Serikali kuwekeza zaidi ya bilioni 20 katika miradi mitatu ya mikubwa ya maji wilani humo.

Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangalla, ameyasema hayo jana kwa nyakati tofauti alipokuwa aklizungumza na wananchi wa kata za Longido na Engarenaibo wilayani Longido, akiwa kwenye ziara ya kukagua uboreshaji wa huduma za afya katika zahanati na vituo vya afya.

Waziri alisema kwa sasa kero namba moja wilayani Longido ni maji na tayari serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa ambao utamaliza tatizo la ukosefu wa maji katika wilaya hiyo.

Waziri Kigwangalla alisema kwa sasa siasa hazina nafasi na badala yake Serikali inatekeleza ahadi zake kwa vitendo ikiwemo hiyo ya kuwapatia wananchi maji na kuwaondolea kadhia ya kutumia muda mwingi kutafuta maji badala kuutumia katika shughuli za kiuchumi.

Amesema wanaotaka siasa wasubiri mwaka 2020 lakini kwa sasa waiache serikali itekeleze miradi kwa ajili ya wananchi kwa kuwa kwenye maendeleo hakuna siasa.

Amesema Serikali pia inaendelea na utekelezaji wa usambazaji umeme vijijini na kufikia mwaka 2021 kila kijiji nchini kitakuwa na umeme na Serikali imejipanga kutekeleza miradi yote lengo ni kuwaondolea wananchi kero za muda mrefu.

Ameongeza kuwa Serikali itatoa shilingi milioni 70 kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha afya cha Engarenaibo ili kiweze kutoa huduma bora zaidi na kwamba Serikali itapeleka watumishi wa afya wilayani humo  ikiwa ni hatua ya kuboeresha huduma za afya.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Longido Godfrey Chongolo, alisema kuwa miradi mitatu ya maji inayotekelezwa katika wilaya hiyo itahakikisha upatikanaji wa maji kwa zaidi ya asilimia mia moja.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na mradi mkubwa wa maji wa Longido wenye thamani ya bilioni 16 ambao utahudumia kata za Olbomba na Engikaret. Miradi mingine ni Gelai Merugoi wenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 na ule wa Kata ya Tingatinga wenye thamani ya shilingi bilioni 1.8.

“Wilaya ya Longido ilikuwa inapata maji chini ya asilimia 20 lakini kukamilika kwa miradi hii kutalifanya tatizo la majikatika wilaya ya Longido kuwa historia kwani maji yatakuwa yanapatikana kwa zaidi ya asilimia mia moja”, alieleza Mkuu wa Wilaya.

Chongolo alieleza kuwa utekelezaji wa miradi miwili ulianza rasmi mara baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani wakati mradi mkubwa wa maji Longido ulianza kutekelezwa mwezi Juni mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo umechangiwa kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa uhakika wa fedha kutoka Serikalini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi