Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), imetakiwa kuendelea kufanya ubunifu ili kuhakikisha inawavutia wasanii kutoka ndani na nje ya nchi kwenda kujifunza fani mbalimbali na kuboresha sanaa zao.
Akizungumza leo Oktoba 12, 2023 alipofanya ziara katika Taasisi hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa amesema kuna baadhi ya wasanii wanafanya kazi nzuri lakini hawana elimu ya sanaa wanazofanya, hivyo wanatakiwa kupewa ushawishi ili kujiunga na mafunzo ya kitaalam.
"TaSUBa ianzishe program mbalimbali zitakazowasaidia wasanii wetu kupata mafunzo ya kitaalam ya namna bora ya kuendesha sanaa zao ili waweze kupanua soko la kazi zao," amesema Bw. Msigwa.
Amesema serikali ipo tayari kuanzisha vituo vya sanaa na utamaduni katika mikoa yote nchini lengo kubwa likiwa kulinda sanaa na utamaduni wa Mtanzania pamoja na maadili ya nchi yetu.