Na Oscar Assenga, Mkinga
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Shirika la Meli Tanzania (TASAC), Captain Mussa Mandia amewataka wafanyabiashara wa mifugo mipakani nchini kutoa ushirikiano kwa wakala huo huku ikiwataka pia kuacha tabia ya kutumia njia za pembeni badala yake wapitishe kwenye mpaka huo ili Serikali iweze kupata mapato yake
Captain Mandia aliyasema hayo leo wakati wa ziara yake ya kutembelea Mpaka huo unaotenganisha kati ya nchi ya Tanzania na Kenya eneo la Horohoro ili kuweza kujifunza na kuona shughuli zinazofanyika kwenye maeneo ya mpaka huo.
Akiwa kwenye mpaka huo, aliwataka wafanyabiashara waongeza ushirikiano ili kuiwezesha Serikali iweze kukusanya mapato yake ikiwemo kuacha kutumia njia za pembeni kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
“Kama leo nipo hapa Mpaka wa Kenya na Tanzania eneo la Horohoro, nimeambiwa usafirishaji mifugo umepungua sana kutoka 10,000 mpaka 3,000 sawa na asilimia 30 ya mifugo sababu kubwa ni ukwepaji wa kupitisha mifugo kwenye kituo hiki kwa sababu mbalimbali
Mwenyekiti huyo wa Bodi alisema wao kama Wakala wataliangalia hilo na kujaribu kuboresha mazingira na kuhakikisha wafanyabiashara wanafaidika na Serikali haipotezi mapato.
“Niwaambie kwamba acheni kutumia njia za pembeni, mkiwa na malalamiko yenu yafikisheni kwetu nasi tutaona namna bora ya kuboresha biashara ya mifugo hapa mpakani”, alisema Mwenyekiti huyo wa Bodi.
Aidha, alionyeshwa kufurahishwa na hatua ya wakala huo mpakani hapo kushirikiana vema na mamlaka nyingine zilizopo Mpakani na kuweza kuboresha makusanyo ya kodi ya nchi yetu yameonekana kwa asilimia 500 ndani ya mwaka mmoja.
Alisema hilo ni jambo muhimu na linahitaji kutazamwa kwa jicho zuri zaidi ili kuweza kuliendeleza na kuongeza wigo mkubwa zaidi ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali.