Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Yatoa Wito kwa Bara la Afrika Kuimarisha na Usalama
Jul 16, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula ametoa wito kwa nchi za Umoja wa Afrika (AU) kuendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na umoja huo katika kutafuta suluhu ya migogoro ili kudumisha amani na usalama barani Afrika. 

Waziri Mulamula ametoa wito huo alipokuwa akichangia ajenda iliyohusu masuala ya nafasi za uanachama katika Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kwenye Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika uliofanyika jijini Lusaka Zambia tarehe 15 Julai, 2022.

Akitoa mchango wake kwa lugha ya Kiswahili Waziri Mulamula alieleza kuwa Tanzania inaunga mkono juhudi zinazofanywa na AU kwa lengo la kuimarisha utendaji wa Baraza la Umoja na Usalama la Umoja wa Afrika ikiwemo kuendelea kuwa na idadi ya wanachama waliopo katika baraza hilo. 

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muumini mkubwa wa usawa wa uwakilishi wa kanda na nchini wanachama ndani ya Umoja wa Afrika na Taasisi nyingine za kimataifa. Hii ni kutokana na imani yetu kuwa endapo usawa utazingatiwa tutaendelea kudumisha umoja na mshikamano wetu ambao kwa muda mrefu umeendelea kuwa nguzo ya amani na usalama katika bara letu”.A lieleza Waziri Mulamula. 

Sambamba na hilo katika Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa ilikuwa ni kupitisha bajeti ya Umoja wa Afrika kwa mwaka 2023. Kitu muhimu katika mkutano huu ni kuwa bajeti hiyo imeweka kifungu kwa ajili ya utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika yaliyopitsha Kiswahili kuwa Lugha ya Kazi ya Umoja wa Afrika. 


Akizungumzia suala hilo Waziri Mulamula ameeleza kuwa amefarijika kuona kipengele maalumu cha kutekeleza maamuzi ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kazi ya Umoja wa Afrika inafanyiwa kazi kwa vitendo. Aliongeza kusema hatua hiyo itaharakisha utekelezaji wa maamuzi hayo kwa kuwa itarahishisha utendaji wa shughuli mbalimbali muhimu kama vile kugharamia zoezi la kutafsiri nyaraka mbalimbali, kulipa au kuajili wakalimani na kuwajengea uwezo wa lugha hiyo wataalamu wa ngazi mbalimbali katika Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Taasisi nyingine za umoja huo. 


Aidha katika mkutano huo wa 41 wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika kwa mara ya kwanza wameandaa baadhi ya taarifa zinazotokana na mkutano huo kwa lugha ya Kiswahili.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi