Tanzania imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambazo zinatekeleza dhana ya ushirikishwaji wa Jamii katika uhifadhi wa kivitendo kwa kutoa fursa kwa wananchi kushiriki moja kwa moja katika kusimamia rasilimali za wanyamapori.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu wa Maliasili na Utalii, Juma Mkomi wakati akifungua warsha ya kupitia na kuthibitisha mkakati wa usimamizi na uendeshaji wa maeneo ya Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori (WMAs) iliyofanyika leo Jijini Arusha.
Amesisitiza kuwa WMAs ni kinga (buffer) muhimu kwa maeneo ya Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Hifadhi ya Ngorongoro na Mapori Tengefu.
Mkomi amesema bila WMAs changamoto za kiuhifadhi zitaathiri moja kwa moja Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Hifadhi ya Ngorongoro na Mapori Tengefu.
Kutokana na umuhimu huo, Mkomi ametoa wito kwa Wadau wa Uhifadhi nchini kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuendeleza WMAs ili kuziwezesha kujisimamia na kujiendesha.
Ameongeza kuwa kupitia ushirikishwaji huo Jamii zimekuwa zikinufaika na matunda yatokanayo na shughuli za uhifadhi katika maeneo yao kwa kujiletea maendeleo na huduma za kijamii ikiwemo shule na zahanati
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dkt. Maurus Msuha amesema toka kuanzishwa kwa dhana ya WMAs jamii imekuwa ikishiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori hali inayopelekea ulinzi wa kuwa madhubuti
Amesema kufuatia hali hiyo maeneo ya WMAs yamekuwa ya kuvutia shughuli mbalimbali za uwekezaji kwa ajili ya utalii wa picha, uwindaji wa kitalii na uwekezaji kwa ajili ya hewa ya ukaa
Akizungumzia manufaa ya ushirikishwaji huo, Dkt. Msuha amesema katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2021 jumla ya jumuiya 15 zenye mikataba ya uwekezaji katika uwindaji wa kitalii zimeweza kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 4.91 ambazo zimewezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ufadhili wa wanafunzi kusoma katika vyuo vikuu