Ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya 68 ya Vito na Usonara katika jiji la Bangkok nchini Thailand, umewavutia wafanyabiashara mbalimbali wa madini kutokana na wengi kutumia malighafi za madini kutoka nchini.
Akizungumza baada ya kushiriki hafla fupi ya ufunguzi wa maonesho hayo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesema wafanyabiashara wakubwa wa madini nchini humo wakiwemo viongozi wa Serikali wameonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali zikiwemo biashara ya madini, uongezaji thamani madini pamoja na kubadilishana uzoefu katika shughuli hizo.
“Uwepo wa Tanzania katika maonesho haya ya madini yenye thamani kubwa unalenga kujifunza pamoja na kuhamasisha urejeshwaji wa minada ya madini nchini na kuhamasisha uwepo wa masoko ya madini ambapo wafanyabiashara wanaweza kununua madini kupitia masoko ya madini yaliyoanzishwa katika kila mkoa nchini”, anaeleza Mbibo.
Ameongeza kuwa, tayari Serikali ya Awamu ya Sita imefungua milango ya biashara katika Sekta ya Madini na kuwataka wadau wa madini nchini kutumia fursa hiyo kuwapokea wawekezaji mbalimbali ili hatimaye kujenga uchumi imara na kuinua ustawi wa watanzania kupitia rasilimali madini.
Akizungumza baada ya ujumbe wa Tanzania kutembelea banda la Kampuni ya Bright Future katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Ashish Baid ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Madini nchini humo na mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite na madini mengine, ameelezea nia yake ya dhati kupitia jukwaa hilo na kampuni yake binafsi ya kushirikiana na Tanzania katika kuipa thamani ya kimataifa minada ya madini endapo Serikali itakuwa yatari kushirikiana nao ikiwemo katika eneo la uongezaji thamani madini.
Naye, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Fine Gamestone Sukharit Sinchawla amesema amefurahishwa na uwepo wa Tanzania katika maonesho hayo na kusema ni nchi nzuri yenye madini mengi mazuri na yenye thamani kubwa na kueleza kwamba ni nchi ambayo kampuni yake inatumia madini mengi kufanya biashara yakiwemo ya Spinel na Tanzanite.
Wadau muhimu wapatao 31 elfu kutoka maeneo mbalimbali duniani wanatarajia kutembelea maonesho hayo kutoka nchi 21 na waoneshaji takribani 1,100. Maonesho ya BangKok yanatajwa kuwa maonesho makubwa na ya kuaminika ambayo wafanyabiashara wachimbaji wanaweza kuyatumia kujenga uhusiano wa kibiashara, kutangaza bidhaa zao na kuuza.