Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Yapiga Hatua Matumizi ya Mtandao- Nape.
Oct 18, 2023
Tanzania Yapiga Hatua Matumizi ya Mtandao- Nape.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akizungumza wakati akifungua kongamano la saba la TEHAMA 2023 leo Oktoba 18, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Na Grace Semfuko, MAELEZO.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuweka mazingira muhimu ya  watumiaji wa mtandao, ambapo idadi yao imeongezeka kutoka watumiaji milioni 29.9 kwa mwezi Aprili 2022 hadi kufikia watu milioni 34.04 kwa mwezi Juni 2023 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 13.

Amesema ongezeko hilo linakwenda sambamba na uhitaji wa wananchi kuelimishwa, kuhusu usalama wa mitandao na namna gani wanaweza kujilinda kwa manufaa yao wenyewe.

Akizungumza wakati akifungua kongamano la saba la TEHAMA 2023, linalofanyika Jijini Dar es Salaam, Waziri Nape amesema kuwepo kwa teknolojia ya kisasa ya mawasiliano, kunawapa nafasi pia watu waovu nao wanatumia fursa za kufanya uhalifu, hivyo amewataka wananchi kuamua kulinda usalama na matumizi ya mtandao.

“Matumizi ya teknolojia zinazoibukia yanakwenda sambamba na uhatarishi wa taarifa zetu binafsi au data mbalimbali zinazokusanywa kwenye teknolojia hizi, hivyo jambo la msingi hususan sasa tukiwa kwenye mwezi wa usalama mtandaoni ni muhimu watumiaji wa huduma za mawasiliano kuzingatia maelekezo ya wataalamu, taratibu na namna za kujilinda na vihatarishi kwenye mitandao, ikiwepo makundi machache ya watu ambao wanatumia mitandao hii kufanya uhalifu”. Amesema Nape.

Aidha amebainisha kuwa, Serikali inatambua jitihada za sekta binafsi za kujenga miundombinu ya mawasiliano, ambapo kupitia mradi wa Tanzania ya kidijitali, ilitia saini mikataba ya kimkakati ya kutoa ruzuku kwa kampuni za mawasiliano yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 275.5 ili kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini na mijini, ambapo jumla ya minara ya mawasiliano 758 katika Kata 713 inajengwa.

Akisoma taarifa za utangulizi kuhusu kongamano hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga, amesema kongamano hilo lilitanguliwa na mikutano miwili ya majadiliano kuhusu mafanikio na changamoto zinazowagusa wanawake na vijana katika sekta ya TEHAMA.

"Hili ni kongamano la siku tano, siku ya kwanza na ya pili, tulijadiliana mafanikio na changamoto zinazowagusa wanawake na vijana katika TEHAMA, tunataka kujenga uchumi wa kidijitali ambao ni jumuishi na tunataka kuangalia makundi haya mawili, tafiti mbalimbali zinaonesha tukiweza kufanya kundi hili wawe na mafanikio, tutapata ukuaji wa TEHAMA vizuri sana, Tanzania ina bahati ya kuwa na vijana wa umri wa kati ya miaka 15-34 wengi ambao ni asilimia 33 ya idadi ya Watanzania wote.” Amesema Dkt. Mwasaga.

Kongamano hilo lilihudhuriwa pia na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, ambapo mwakilishi wa kamati hiyo, Mhe. Livingstone Lusinde, amesema kutokana na kukua kwa kasi ya teknolojia, wanaona kuna kila sababu ya kamati hiyo kuunga mkono juhudi za Serikali, katika usimamizi na uchambuzi wa sheria mbalimbali mpya zitakazopelekwa bungeni, ikiwa ni pamoja na kuomba ongezeko la bajeti ya sekta ya TEHAMA. 
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi