Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Yaihakikishia Jumuiya ya Kimataifa Uchaguzi Huru na wa Haki
Feb 26, 2020
Na Msemaji Mkuu

  [caption id="attachment_51233" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) (katikati aliyeshika kalamu) akiwa katika mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Scotland. Kushoto kwa Prof. Kabudi ni Balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Geneva,Uswisi Balozi Maimuna Tarishi pamoja na Wakurugenzi na Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Jumuiya hiyo zilizopo Geneva,Uswisi[/caption]

Tanzania imesema hatua zote ambazo zimechukuliwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya mabadiliko katika sheria za vyama vya siasa,sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali na ile ya vyombo vya habari ina lengo la kuimarisha uwajibikaji na uwazi pamoja na kuhakiskisha misingi na tunu za Taifa zinaheshimiwa na kuendelezwa.

Akihutubia katika Kikao cha 43 cha Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa linaloendelea Geneva nchini Uswisi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ameihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa Tanzania  inaheshimu na itaendelea kuheshimu haki zote binadamu zikiwemo za kisiasa na kwamba sheria zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zina lengo jema la kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa Taifa lenye amani,umoja na utulivu.

Pia Prof. Kabudi ameifahamisha jumuiya ya Kimataifa kuwa mwaka huu Tanzania itafanya uchaguzi wake mkuu wa sita tangu kuanzishwa kwa vyama vingi vya siasa na kuihakikishia jumuiya hiyo kuwa uchaguzi huo utakuwa wa uwazi,huru na wa haki na kwamba Tanzania itaalika waangalizi mbalimbali wa uchaguzi watakaotaka kushuhudia namna Watanzania wanavyotekeleza moja ya haki zao za msingi katika suala la kidemokrasia  kwa kuchagua viongozi wao.

[caption id="attachment_51234" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Scotland akiwa katika mazungumzo na Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) (hayupo pichani) Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Jumuiya hiyo zilizopo Geneva,Uswisi. Kulia ni msaidizi wa Bi Patriacia Scotland.[/caption]

Kuhusu masuala ya sheria mpya za huduma vyombo vya habari,na haki ya kupata taarifa Prof. Kabudi ameiambia jumuiya ya kimataifa kuwa sheria hizo mpya  zilizotungwa na Bunge la jamhuri ya Muungano ina lengo la kuimarisha,kulinda na kuweka mazingira bora zaidi kwa waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa usalama na kwa kuzingatia taaluma sambamba na kuwawezesha kupata haki zao ikiwa ni pamoja na mishahara bora na mikataba ya kazi.

Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Patricia Scotland mazungumzo yaliyolenga masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na mradi ambao Jumuiya ya Madola umeufanya kuhusu Tanzania.

[caption id="attachment_51235" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Scotland mara baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Jumuiya hiyo zilizopo Geneva,Uswisi. Kushoto kwa Bi. Patricia Scotland ni Balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Geneva,Uswisi Balozi Maimuna Tarishi[/caption]

Mradi huo umelenga kuangalia takwimu mbalimbali zinazohusu biashara kwa kuangalia nchi ambazo Tanzania inaagiza ama kuuza bidhaa zake kwa wingi katika nchi za Jumuiya ya Madola mradi ambao umeelezwa kuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania ambapo kwa sasa nchi za India na Afrika kusini ndizo kinara.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Bi Patricia Scotland amesema Tanzania ni mdau muhimu katika jumuiya hiyo na kwamba amefurahi kumkabidhi Prof. Kabudi nakala ya utafiti huo kwa niaba ya Tanzania jambo litakaloifanya Tanzania kuendelea kuangalia maeneo ya kujiimarisha katika ufanyaji wa biashara na nchi za Jumuiya ya Madola.

Mbali na masuala hayo ya mradi huo wa takwimu wa biashara kuhusu Tanzania uliofanywa bure na Jumuiya hiyo ya Madola pia wawili hao wamezungumzia masuala mengine ikiwa ni pamoja na namna Jumuiya hiyo na Tanzania zitakavyofanya kuongeza usawa wa jinsia,masuala ya haki za binadamu pamoja na uimarishaji wa mfumo wa mahakama nchini Tanzania.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi