Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Yaanza Kufikia Mabadiliko Endelevu ya Kidijitali
Sep 29, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Innocent Mungy, Bucharest

Tanzania inatekeleza mfumo wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali ambao utahakikisha sekta zote za uchumi zinatumia TEHAMA huku ikiwezesha mabadiliko ya kidijitali yanayojenga jamii jumuishi ya kidijitali kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Hayo yalisemwa na Mheshimiwa Nape Nnauye (Mbunge), Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakati akiwasilisha Tamko la Kisera la Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Mawasiliano Duniani (ITU PP 2022) unaofanyika hapa Bucharest, Romania.

Mheshimaiwa Nape alisema Tanzania ina Sera ya Taifa ya TEHAMA, ambayo imesababisha ongezeko kubwa la matumizi ya TEHAMA katika sekta mbalimbali za uchumi. Tanzania pia imewezesha ujumuishaji wa kifedha ambao umehusisha idadi ya watu wa Tanzania ambao hawakuwa wanapata huduma za kibenki hasa jamii ya vijijini. Alihusisha mafanikio hayo na ushiriki wa Sekta Binafsi.

"Tangu tuanzishe Mfumo wa Leseni uliounganishwa mwaka 2005 ili kuinua TEHAMA katika jitihada zetu za kuinua ustawi wa kijamii na kiuchumi wa watu wetu, tumeona mafanikio. Shukrani kwa mikakati ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Tanzania imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika suala zima la ujumuishaji wa kifedha (Financial Inclusion). Leo hii kuna zaidi ya watumiaji milioni 35.75 wa huduma za fedha kupitia simu ikilinganishwa na watumiaji milioni 23.34 mwaka 2018" alisema Mhe. Nape Nnauye.

Serikali ya Tanzania imewekeza maelfu ya kilomita za Mkongo wa Taifa wa TEHAMA (NICTBB).  Mheshimiwa Nnauye alisema kuwa mipango ya uunganishaji wa Mkongo wa Mawasiliano kwa nchi jirani na zisizo na bandari ni ahadi ambazo Tanzania imekuwa ikizipa kipaumbele sana. Mkongo wa Taifa unaunganisha nchi zisizo na Bahari kupitia maeneo ya mpakani ya Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC, Zambia na Malawi. Mkongo huu una urefu wa KM 18,000.

"Ili kupata mitandao ya mawasiliano, mifumo ya habari na upatikanaji wake, Tanzania imeanzisha Timu yake ya Taifa ya Kukabiliana na Dharura ya Usalama wa Kompyuta (TZ-CERT) ili kuratibu matukio ya kimtandao katika ngazi ya kitaifa" alieleza Mheshimiwa Nape Nnauye.

Katika kuhakikisha nchi nzima inaunganishwa katika mawasiliano, Tanzania imeanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (USCAF). Hadi sasa Mfuko umeweza kuunganisha vijiji 316 vyenye wakazi 730,000.  

"Serikali iliweka malengo mazuri ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma za intaneti yenye kasi na huduma kwa asilimia 80 kitaifa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2024" alisema Mhe.

Zaidi Mheshimiwa Nape alisema usambazaji wa huduma za mawasiliano kwa kila sehemu nchini ili kuziwezesha jamii za vijijini upatikanaji wa simu za mkononi unaendelea vizuri. Mfuko wa Mawasiliano kwa wote pia umeanzisha miradi mingine ikiwa ni pamoja na kuunganisha shule, vituo vya mawasiliano na miradi mingine mingi.

Akizungumzia Tanzania kugombea nafasi katika Baraza Kuu la ITU kwa mwaka 2023-2026, Mheshimiwa nape amesema uzoefu wa Tanzania katika Sekta ya Mawasiliano unaweza kuwa wa manufaa zaidi kwa familia ya ITU kama mjumbe wa Baraza la ITU hasa katika kipindi hiki ambapo sekta ya Maasiliano inabadilika kwa kasi, na jumuiya ya kimataifa iko tayari zaidi kutumia bidhaa na huduma za teknolojia ya habari na mawasiliano kama zana ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

"Napenda kusisitiza kuwa Tanzania imedhamiria kushirikiana na nchi nyingine wanachama, Sekretarieti ya ITU kuifanya ITU kuwa chombo muhimu cha kimataifa ambacho kina mchango mkubwa katika kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi zote wanachama" alifafanua zaidi Mhe.Nnauye.

Tanzania inagombea kiti cha Baraza Kuu la ITU linalowakilisha eneo D la Afrika. Mheshimiwa Nape amewaomba wanachama wote wa ITU waipigie kura Tanzania katika Baraza la ITU, ili iweze kubadilishana uzoefu na familia nzima ya ITU na kuchangia zaidi Dira na Ujumbe wa ITU.  Mheshimiwa Nnauye amesema Tanzania inashirikiana kwa karibu na ITU kuhakikisha matumizi ya mawasiliano ya simu na TEHAMA kwa wananchi wote wa Tanzania na msisitizo zaidi kwa wanawake na wasichana, vijana, wazee na watu wenye ulemavu.

Uchaguzi wa baraza Kuu la ITU unatarajiwa kufanyika tarehe 3 Oktoba, 2022, ambapo Tanzania na nchi zingine 16 zinawania nafasi 13 kuwakilisha bara la Afrika. Baraza hilo lina jumla ya wajumbe 48.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi