Serikali ya Tanzania na Urusi zimekubaliana kuongeza maeneo ya ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji, utalii pamoja na utamaduni.
Makubaliano hayo yamefikiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa Urusi nchini, Mhe. Andrey Levonovish Avetsyan katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Balozi Mbarouk amesema kuwa Tanzania na Urusi zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu wa kihistoria ambao uliasisiwa na Waasisi wa Mataifa hayo mawili, “ kutokana na uhusiano mzuri tulionao umechangia kuimarisha sekta ya utalii, elimu pamoja na afya,” alisema Balozi Mbarouk.
Balozi Mbarouk aliongeza kuwa Tanzania na Urusi zitaendelea kujikita zaidi kufungua maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji, utalii na masuala mengine ya kiuchumi kwa maslahi mapana ya mataifa hayo.
Kwa upande wake Balozi wa Urusi nchini, Mhe. Andrey Levonovish Avetsyan ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano ambao imekuwa ikimpatia tangu alivyowasili na kuongeza kuwa Urusi itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuendeleza ushirikiano wa kufanya kazi kwa pamoja kwa manufaa ya mataifa mawili.
“Naamini kuwa mimi ni kiungo cha kuimarisha na kuendeleza uhusiano baina ya Urusi na Tanzania, tumekuwa tukishirikiana katia sekta mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, elimu na afya utalii na utamaduni naahidi kuwa Urusi itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” Amesema Balozi Avetsyan
Balozi Avetsyan ameongeza kuwa katika mwaka huu Serikali ya Urusi imepanga kutoa fursa za masomo kwa wanafunzi wa kitanzania takribani 70.