Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania, Qatar Kuendeleza Ushirikiano – Waziri Ndalichako
Feb 19, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Tanzania imekusudia kuendeleza uhusiano uliopo kati yake na nchi ya Qatar sambamba na kukuza mahusiano ya kibiashara, uchumi na fursa za ajira.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako alipokuwa na mazungumzo na ugeni kutoka nchi ya Qatar ambapo kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Mkutano uliopo hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam Februari 18, 2022.

Waziri Ndalichako ameeleza kuwa, Tanzania na Nchi ya Qatar zimekuwa na mahusiano mazuri kwa muda mrefu na mataifa hayo yamekuwa yakishirikiana katika mambo mengi ikiwemo Biashara, Uwekezaji na shughuli nyingine nyingi zenye manufaa kwa nchi hizo mbili.

“Niipongeze Nchi ya Qatar kwa kuonyesha dhamira ya dhati katika utekelezaji wa makubaliano tuliyoingia tangu mwaka 2014 ambao umelenga kuimarisha uhusiano wa nchi zetu katika nyanja mbalimbali zenye maslahi ya pande zote mbili,” alisema Prof. Ndalichako.

Aliongeza kuwa, tangu Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Samia Suluhu Hassan aingie madarakani amekuwa akionyesha dhamira yake ya dhati katika kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na mataifa mengine na pia amekuwa akifungua fursa za uwekezaji nchini, ufanyaji wa biashara sambamba na kuwezesha watanzania kushirikiana na nchi rafiki katika nyanja mbalimbali. 

Wakati huo huo, Waziri Ndalichako aliipongeza nchi ya Qatar kwa kuwa wenyeji wa Kombe la Dunia, hivyo alitumia fursa hiyo kuhamasisha ushirikishwaji wa vijana wa kitanzania katika fursa mbalimbali za ajira zitakazotolewa kuelekea katika maandalizi ya michuano hiyo.

“Tunafahamu mwaka huu 2022 nchi ya Qatar itakuwa mwenyeji wa michuano wa Kombe la Dunia, hivyo mtambue kuwa nchi yetu imeendelea kuwaandaa vizuri sana vijana wake ili waweze kuwa na ujuzi ambao unahitajika katika nyanja mbalimbali ambao utawawezesha waweze kuajirika,” alisema

Sambamba na hayo Mhe. Ndalichako alieleza kuwa Serikali imeendelea kuratibu vyema na kuzingatia misingi katika kupeleka watanzania kufanya kazi katika maeneo mbalimbali ya nje nchi.

Pia alieleza kuwa, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikiratibu Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ambayo imekuwa ni chachu ya kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa fani mbalimbali zinazohitajika nchini pamoja na kwenye mataifa mengine. 

Naye, Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Kazi Qatar, Mhe. Mohamed Hassan al Obaidali ameeleza kuridhishwa na mazingira yaliyopo nchini na ukarimu wa Watanzania na kuahidi kuwa wa Serikali ya nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuangalia uwezekano wa kuwekeza kwenye miradi ya kiuchumi itakayoziletea maendeleo nchi hizo mbili.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi