Tanzania na Malawi zimeweka nia ya kushirikiana katika usafiri kwa njia ya barabara, huduma za Bandari katika ziwa Nyasa na uhudumiaji wa mizigo ya Malawi katika Bandari ya Dar es Salaam.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Uchukuzi, Gabriel Migire kwenya Mkutano uliowakutanisha Makatibu Wakuu wa sekta ya Uchukuzi toka Tanzania na Malawi ambapo lengo la Mkutano huo ni kuboresha usafirishaji kwa njia ya barabara,
“Tumewekeana nia ya kushirikiana katika huduma za Bandari kwa ziwa Nyasa kwa kuwa ziwa hili lipo katika pande mbili yaani Tanzania na Malawi pia kuendelea kuwashawishi kutumia Bandari ya Dar es Salaam”, alisema Migire.
Kwa Upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Usafirishaji wa Umma kutoka Malawi, Hastings Chiudzu amesema kuwa ni muhimu kwa wizara hizi kushirikiana na kuondoa changamoto mbalimbali za usafirishaji
Pia, Katibu Mkuu huyo amesema ataendelea kuwashawishi wafanyabishara wa Malawi kuendelea kutumia Bandari ya Dar es Salaam kwani Bandari hii ina utaratibu mzuri wa kushusha na kupakia mizigo.
Wataalam hao kutoka Malawi walitembelea ujenzi wa SGR na Bandari ya Dar Es Salaam na kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutekeleza mradi huo mkubwa wa ujenzi wa SGR pamoja na upanuzi wa Bandari.