Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa, Serikali ya Tanzania na Malawi zimeanza majadiliano ili kuona uwezekano wa kujenga mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya Maji ya Mto Songwe pamoja na kuendeleza rasilimali za mto huo.
Mhandisi Mramba amesema hayo wakati akifungua kikao cha majadiliano kuhusu mradi huo kati ya wataalam kutoka Wizara za Nishati upande wa Tanzania na Malawi unaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili kuanzia Agosti 9 na 10, 2023.
Amesema kuwa, majadiliano hayo kwa siku ya kesho yatahusisha Mawaziri wa Nishati, Makatibu Wakuu na Maafisa kutoka Wizara za Nishati za nchi hizo mbili ambapo endapo wataridhia na kukubaliana na majadiliano husika watasaini makubaliano ya kuanza mradi huo.
“Majadiliano katika kikao hicho yanalenga katika kuendeleza rasilimali za pamoja katika nchi hizo mbili hasa uwezekano wa kujenga mtambo wa kuzalisha umeme katika mto Songwe na pia uwezekano wa kutumia mto huo kuwa chanzo cha matumizi ya maji na umwagiliaji katika eneo la mpaka wa Tanzania na Malawi”, amesema Mramba.
Ameongeza kuwa, majadiliano hayo pia yanahusu uwezekano wa kujenga njia ya kusafirisha umeme itakayounganisha nchi hizo mbili za Tanzania na Malawi.
Mramba amesema njia hizo za kusafirisha umeme zitajengwa kwa kuzingatia hali ya upatikanaji wa umeme kwa pande zote mbili kwa maana njia hizo zitakuwa na uwezo wa kusafirisha na kusambaza umeme kutoka nchi moja kwenda nyingine ikiwa moja wapo itakuwa imepata changamoto ya kukosa umeme.
Ameeleza kuwa, mpango wa Tanzania katika sekta ya nishati ni kuiunganisha nchi hiyo na nchi zote zilizo jirani yake.
Mkutano huo pia utajadili mashirikiano katika sekta nyingine za nishati kama Gesi Asilia ikiwemo kuangalia uwezekano wa kujenga bomba la kusafirisha Gesi Asilia kutoka Tanzania kwenda Malawi na mipango mingine inayohusisha Gesi na Mafuta.
Ufunguzi wa kikao hicho umehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Viongozi Waandamizi kutoka Shirika na Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na maafisa kutoka taasisi zilizo chini ya Wizara.