Na: Paschal Dotto
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China zinaendelea kuboresha na kuimarisha ushirikiano na mahusiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Lilly Beleko kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel wakati wa uzinduzi wa tamasha la urithi wa utamaduni usioshikika uliofanyika katika kituo cha utamaduni Jijini Dar es salaam.
Bi. Beleko amesema kuwa utamaduni ni kiunganishi muhimu katika kubadilisha uzoefu, ushirikiano na kujenga mahusiano kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumzia uimara wa ushirikiano kati ya China na Tanzania, Bi Beleko amesema kuwa uhusiano umezidi kuimarika kwa kuzingatia mkataba wa kiutamaduni wa uliosainiwa hivi karibuni. Aidha, Serikali ya China inatoa nafasi 200 kila mwaka kwa Watanzania kwenda kusoma nchini China hatua ambayo inasaidia wanafunzi na maofisa mbalimbali wa Tanzania kuongeza ujuzi na maarifa katika kutekeleza majukumu yao.
Kwa upande wa Mikataba ya Kimataifa, Bi Beleko amesema kuwa Mkataba wa Urithi wa Utamaduni Usioshikika wa UNESCO wa mwaka 2003 ambao unasisitiza uwepo wa maelewano na kuheshimu utamaduni wa mtu mwingine kama inavyojulikana kwamba utamaduni ni imani na itikadi za mtu katika sehemu mbalimbali ikiwemo itikadi za kisiasa na kidini.
“Lengo la mkataba wa UNESCO ni kuondoa migogoro, mikwaruzano kutokuelewana na hata vita kwani kila mtu ataheshimu urithi wa utamaduni wa mwingine” alisema Bi Beleko
Akizungumzia Kutuo cha Utamaduni cha China Kikilichopo nchini Bi Beleko amesema “Kituo hiki kwa Tanzania kinatoa mchango mkubwa na mafanikio katika kutunza na kudumisha urithi wa utamaduni usioshikika kwani Jamhuri ya Watu wa China wako katika hali ya juu sana katika kutafiti, kukusanya, kuorozesha, kuhifadhi, kuenzi na kurithisha utamaduni wake kwa vizazi vya badae”.
Zaidi ya hayo utamaduni ni moja sekta inayokua kwa kasi hatua ambayo inasaidia katika kuongeza vituo vya utalii hatua inayoongeza fursa katika sekta ya utalii nchini
Naye Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Dkt. Lu Youqing ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kudumisha mahusiano ya kidplomasia kwa miaka mingi tangu kuasisiwa kwake.
Aidha, Balozi Lu amesema kuwa Tanzania inaumuhimu kwa Jamhuri ya Watu wa China ambapo katika kuimarisha mahusiano kwa kutoa nafasi 200 kwa Watanzania kwenda kusoma nchini China.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje ya Wizara ya Utamaduni wa China ameipongeza Wizara ya Utamaduni, Sana na Michezo kwa ushirikiano mzuri hasa katika uzinduzi wa wiki ya urithi wa utamaduni wa China ambao unasimamiwa katika mji wa urithi na asili ya utamaduni China Ningxia na kuwakaribisha Watanzania kutembelea mji huo wenye maajabu mbalimbali na kama utamduni wa China, mito, milima, vijito na mabonde ambayoni vivutio vya utalii.
Mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China yalianza rasmi mwaka 1964 ikiwa na dhamira ya kuinua uchumi katika nchi hizi mbili na kuisaidia Serikali ya Tanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi pamoja na teknolojia.