Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Kuuza Nyama Tani 16,000 Ifikapo 2026
Oct 28, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Serikali imedhamiria kuongeza kiwango cha uuzaji wa nyama nje ya nchi na kufikia tani 16,000 ifikapo mwaka 2026 kwa lengo la kuendeleza ukuaji wa tasnia ya nyama na kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.

Hayo yameelezwa na Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania, Dkt. Daniel Mushi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya bodi hiyo pamoja na vipaumbele vyake.

“Tumedhamiria kuongeza kiasi cha nyama kinachouzwa nje ya nchi kwa kushirikiana na Viwanda vya Nyama na wafanyabiashara wanaouza nyama nje kuweka mikakati ya kulinda masoko ya nyama tuliyonayo ambapo kwa sasa tunauza nyama Qatar, UAE, Bahrain, Kuwait, Oman, Comoro, Hong Kong, Jordan, Saudi Arabia. Mwaka 2021 tumeuza tani 10,415 zenye thamani ya shilingi milioni 42 za kimarekani na robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2022/23 tumeuza tani 3,256.60 za nyama nje ya nchi zenye thamani ya dola za marekani milioni 13 na lengo letu ni kuuza tani 16,000 ifikapo 2026”. Amesisitiza Dkt. Mushi.

Aidha, Dkt. Mushi ametaja baadhi ya manufaa watakayopata wananchi kutokana na utekelezaji wa vipaumbele vya kazi zinazofanywa na Bodi hiyo kuwa ni kuongezeka kwa ubora na usalama wa nyama inayopatikana sokoni na kulinda afya za wananchi kupitia mafunzo yanayotolewa na Bodi ya Nyama na ukaguzi wa kazi za wadau.

Aidha, upatikanaji wa soko la uhakika la mifugo kutokana na viwanda vya nyama kuongeza uzalishaji na ongezeko la fursa za ajira kupitia sekta ya mifugo haswa kwa vijana kufanya unenepeshaji wa mifugo na kuingia mikataba na viwanda vya kuchakata nyama kunatajwa kuwa na manufaa kwa wananchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi