Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Kunufaika na Msaada wa Dola Bilioni 30 Zilizoahidiwa na China
Aug 19, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema kuwa Serikali ya Tanzania inatarajia kunufaika na mpango wa msaada wa miaka mitatu utakaogharimu Dola za Marekani bilioni 30, ulioahidiwa na Rais wa jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa XI JINPIN, wa kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na umasikini.


Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam alipofanya mazungumzo kwa njia ya mtandao na Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Qian Keming, wakati wa mkutano wa 6 wa Kamati ya Pamoja ya Uchumi, Ufundi na Biashara kati ya Tanzania na China.


Alisema kuwa msaada huo ulioahidiwa na Rais wa nchi hiyo, Mheshimiwa XI Jinping, mwezi Novemba mwaka 2021, Mjini Dakar, Senegal, kupitia mpango wa ushirikiano wa China na Afrika wa mwaka 2035, utasaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.


Dkt. Nchemba alisema kuwa kupitia mpango huo, miradi 9 imekusudiwa kutekelezwa katika sekta za afya, kilimo, kutokomeza umasikini, kuendeleza biashara, uwekezaji, ubunifu wa teknolojia, kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi, kujenga uwezo na uhusiano wa moja kwa moja wa watu wa nchi hizo mbili.


“Tumewasilisha China miradi kadhaa ya kimkakati na kipaumbele ili nchi hiyo iweze kuisadia Tanzania kupata misaada na mikopo nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo itakayosaidia kukuza uchumi wa nchi na kuwaondolea wananchi wake umasikini, tunaamini tutapata fedha hizo” alisema Dkt. Nchemba.


Aidha, Dkt. Nchemba aliishukuru China kwa misaada mbalimbali iliyochangia kufanikisha miradi mbalimbali hapa nchini ikiwemo miundombinu ya reli, elimu, tehama, nishati, maji, kilimo, maendeleo ya viwanda pamoja na afya na kwamba misaada hiyo itaendelea kutolewa ili kuiwezesha nchi kukabiliana na umasikini na kukuza uchumi wake.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Qian Keming, aliahidi kuwa nchi yake itaendeleza uhusiano na ushirikiano na Tanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii ili iweze kutimiza malengo yake ya kupiga hatua kiaendeleo na kuboresha maisha ya watu wake.


Alisema kuwa China itaendelea kuhamasisha uwekezaji kwa kuzishawishi kampuni kutoka nchini humo kwenda kuwekeza Tanzania pamoja na kusaidia kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.


Mheshimiwa Keming alielezea kufurahishwa na kuongezeka kwa biashara kati ya Tanzania na China, hususan katika biashara ya mazao ikiwemo zao la muhogo na kwamba jitihada zaidi zinatakiwa ili Tanzania iweze kunufaika na soko la China kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula yanayohitajika kwa wingi nchini mwake.


Mkutano huo umewashirikisha Mawaziri kadhaa wa Kisekta pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Salum Mkuya, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, na maafisa kadhaa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi