Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Kuendelea kuimarisha biashara na Malawi
Jun 08, 2018
Na Msemaji Mkuu

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, kulia akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Malawi litakalofanyika Julai 26 na 27 jijini Mbeya, kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) John Mnali.

Na Fatma Salum-MAELEZO

Serikali ya Tanzania inaendelea na jitihada za kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na Serikali ya Malawi kupitia sekta ya biashara na uwekezaji ili wananchi waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana katika nchi zote mbili. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, leo Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla alisema kuwa katika kuimarisha uhusiano huo, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Malawi zimeandaa Kongamano la Biashara na Uwekezaji litakalofanyika Julai 26 na 27 mwaka huu Jijini Mbeya. Makalla alieleza kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji wan chi zote mbili ili kubaini fursa mbalimbali zitakazowezesha kuanzisha na kuendeleza miradi katika sekta za viwanda, usafirishaji, utalii, uvuvi, kilimo, madini, elimu, afya, benki, mawasiliano, Tehama na biashara kwa ujumla.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, kulia akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Malawi litakalofanyika Julai 26 na 27 jijini Mbeya.

“Kongamano hili linatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki wapatao 500 ikijumuisha wafanyabiashara, wawekezaji, Taasisi za Umma na sekta binafsi kutoka Tanzania na Malawi,” alisema Makala.

Sambamba na kongamano hilo, kutakuwepo mikutano ya wafanyabiashara (B2B), mikutano ya watendaji wa Serikali (G2G) na mikutano kati ya Serikali na wafanyabiashara (B2G) kutoka nchi zote mbili.

Makalla alisisitiza kuwa Mkoa wa Mbeya uko tayari kuchangamkia fursa za kibiashara na Malawi kwa sababu miundombinu ipo ya kutosha ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, meli mbili za kubeba mizigo ambazo zimeshaanza kufanya kazi na meli moja ya abiria ambayo itakamilika Julai mwaka huu.

Baadhi ya watendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla (hayupo pichani) kuhusu kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Malawi litakalofanyika Julai 26 na 27 jijini Mbeya.

Aidha, alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kuanza ujenzi wa kituo kimoja cha forodha (One Stop Boarder Post) katika mpaka wa Kasumulu na imetenga eneo la kujenga bandari kavu katika eneo la Inyala kwa lengo la kuwezesha upokeaji na uhifadhi wa bidhaa moja kwa moja kutoka bandari ya Dar es Salaam.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), John Mnali alisisitiza kuwa kongamano hilo ni muhimu kwa wafanyabiashara wa kitanzania hivyo wajitokeze kushiriki ili waweze kuibua fusra mpya na kujitangaza kwa wenzao wa Malawi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini, Godfrey Simbeye, kulia akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Malawi litakalofanyika Julai 26 na 27 jijini Mbeya.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alitoa wito kwa wafanyabiashara wote hasa sekta binafsi kujitokeza kwa wingi kuangalia fursa zilizopo Malawi na kubadilishana uzoefu wa kibiashara.

Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji (TIC), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade) na Taasisi ya Biashara na Uwekezaji ya Malawi (MITC) wanaratibu kongamano hilo na mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Rais wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini, Godfrey Simbeye, kulia akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Malawi litakalofanyika Julai 26 na 27 jijini Mbeya, katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya , Amos Makalla na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) John Mnali.

(Picha na Eliphace Marwa - Maelezo)

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi