Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania, Korea Kusini Kuunganisha Nguvu Sekta ya Madini
Sep 03, 2023
Tanzania, Korea Kusini Kuunganisha Nguvu Sekta ya Madini
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde akizungumza katika mkutano baina ya Serikali ya Tanzania chini ya Wizara ya Madini na ujumbe kutoka Korea Kusini uliojumuisha viongozi wa Makampuni makubwa ya madini yanayohusika na mnyororo wa thamani wa uzalishaji betri za magari na kujadili kuhusu ushirikiano katika uendelezaji wa madini ya kimkakati nchini Tanzania.
Na Wizara ya Madini

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde ameishukuru Serikali ya Korea Kusini kwa kuichagua Tanzania na kufanya mazungumzo kuhusu uwekezaji katika Sekta ya Madini hivyo kuunganisha nguvu katika kuiinua sekta hiyo

Ameyasema hayo Septemba 2, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika mkutano baina ya Serikali ya Tanzania chini ya Wizara ya Madini na ujumbe kutoka Korea Kusini uliojumuisha viongozi wa Makampuni makubwa ya madini yanayohusika na mnyororo wa thamani wa uzalishaji betri za magari na kujadili kuhusu ushirikiano katika uendelezaji wa madini ya kimkakati nchini Tanzania.

"Tanzania inaweka kipaumbele katika uchimbaji wa Madini Mkakati kwa kufanya tafiti za madini hayo ili kuendana na soko hilo duniani, vilevile miradi mbalimbali ya Madini Mkakati inaendelea kutekelezwa katika Sekta ya Madini ikiwemo ya Lindi Jumbo na Kabanga Nikeli", alisema Waziri  Mavunde.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini humo, Togolani Mavura alieleza kuwa ushirikiano kati ya Korea Kusini na Tanzania unazidi  kuimarika na imani yake kuwa mada zilizowasilishwa na wataalam kutoka Wizara ya Madini kuhusu fursa zilizopo zimeongozea uelewa juu ya sekta hiyo.

Pia, Mjumbe Maalum wa Rais wa Korea ambaye ndiye kiongozi wa ujumbe huo kutoka Korea Kusini, Bw. Yoon Sang Jick aliishukuru Serikali ya Tanzania na kuahidi kuwa wataendelea kushirikiana nayo kuhakikisha malengo ya uwekezaji yanafanikiwa.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Watendaji Wakuu kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE).

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi