Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania, Hungary Kushirikiana Sekta ya Elimu
Jul 19, 2023
Tanzania, Hungary Kushirikiana Sekta ya Elimu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dtk. Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake Rais wa Hungary, Mhe. Katalin Novák (hayupo pichani) wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Julai, 2023. Rais Novák yupo nchini Tanzania kwa ziara ya siku tatu.
Na Lilian Lundo - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Hungary, Mhe. Katalin Novák wamekubaliana kushirikiana katika sekta ya elimu ili kuhakikisha vijana kutoka nchi hizo mbili wanapata nafasi ya kusoma zaidi nje ya nchi zao.

Viongozi hao wamesaini makubaliano leo Julai 18, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam walipokuwa wakiongea na Vyombo vya Habari.

“Kwa upande wa elimu, nchi ya Hungary ni washirika muhimu kwa Tanzania hasa katika kuinua elimu ya juu, kwa pamoja tumeweza kukuza ushirikiano wetu katika elimu. Tumeshuhudia utiaji saini wa makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wetu katika sekta ya elimu,” amesema Rais,  Mhe. Samia.

Rais wa Jamhuri ya Hungary, Mhe. Katalin Novák akizungumza na Waandishi wa Habari Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Julai, 2023.

Kwa upande wake Mhe. Rais Novák amesema kuwa Hungary wana programu zinazofadhiliwa na Serikali, ambapo kuna wanafunzi 12,000 kutoka nchi 19 wanaosoma Hungary kupitia programu hiyo wakiwemo Watanzania.

“Makubaliano yetu ya leo, yametoa nafasi kwa wanafunzi wa Hungary kuja kusoma Tanzania na kujifunza lugha za Tanzania, watakuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania watakaporudi Hungary baada ya masomo yao,” amesema Mhe. Rais Novák.

Aidha amemshukuru Rais Samia kwa kutoa nafasi ya wanafunzi kuja kusoma Tanzania, ambapo pia watapata fursa ya kujifunza tamaduni mbalimbali za Kitanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Hungary, Mhe. Katalin Novák wakishuhudia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu kutoka Hungary, Tristan Azbej aliyeiwakilisha Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Nchi hiyo wakati wakisaini Hati ya Makubaliano baina ya nchi mbili kuhusu Ushirikiano wa ndani wa Programu ya Stipendium Hingaricum ya mwaka 2024-2026, Ikulu Jijini Dar es Salaam.   Stipendium Hingaricum ni Programu ya ufadhili wa masomo ya Elimu ya Juu (Scholarship) inayotolewa na Serikali ya Hungary kwa ajili ya wanafunzi wa kigeni.

Marais hao pia wamekubaliana kushirikiana katika kukuza uchumi wa nchi zote mbili, ambapo wamekubaliana kuwa na jukwaa la biashara mapema mwakani ambalo litashirikisha wadau wa biashara kutoka Tanzania na Hungary, ili kuboresha uchumi pamoja na kuangalia maeneo ya uwekezaji wa viwanda.

Rais wa Hungary, Mhe. Katalin Novák yuko nchini Tanzania kwa ziara ya siku ya nne ambapo anatarajia kutembelea Hifadhi ya Ngorongoro na baadhi ya maeneo ya Kilimanjaro.
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi