Tanzania na Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi wa Umoja wa Falme za Kiarabu, zimetiliana saini mkataba wa mkopo nafuu wa Dola za Marekani milioni 30 sawa na shilingi bilioni 70 za Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme Msongo wa kV 220 kutoka Benaco hadi Kyaka na upanuzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Kyaka mkoani Kagera.
Mkataba huo umetiwa saini katika Makao Makuu ya Mfuko huo Mjini Abu Dhabi na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa niaba ya Serikali, na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (Abu Dhabi Fund for Development), Mhe. Mohammed Saif Al Suwaidi.
Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme umbali wa kilometa 167 kutoka Benaco hadi Kyaka na kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, hadi mradi huo utakapokamilika unatarajia kugharimu Dola za Marekani milioni 119.4.
“Mkopo huu tuliosaini utachangia nguvu zilizotolewa na Mifuko mingine ukiwemo OPEC Fund for International Development uliotoa Dola za Marekani milioni 60, Mfuko wa Maendeleo wa Saudia uliotoa Dola za Marekani milioni 13 na Serikali ya Tanzania iliyochangia Dola za Marekani milioni 2.4” Alisema Dkt. Nchemba
Imeelezwa kuwa, kukamilika kwa mradi wa umeme wa Benaco-Kyaka, kutaimarisha hali ya upatikanaji umeme katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo kumekuwa na changamoto ya kuwepo kwa umeme pungufu na usio wa uhakika na pia kuufanya Mkoa wa Kagera kuanza kutumia umeme wa Gridi ya Taifa badala ya kutumia umeme kutoka nchi jirani ya Uganda.
Dkt. Nchemba aliupongeza Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuwaletea wananchi maendeleo kupitia miradi ya nishati ambao utakuza uchumi na ajira kwa wakazi wa maeneo ambayo umeme utapitishwa.
“Mpaka sasa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi umewekeza nchini Tanzania kiasi cha Dola za Marekani milioni 96.6 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii na umekuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya nchi kwa muda mrefu” aliongeza Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi, Mhe. Mohammed Saif Al Suwaidi amesema kuwa Mfuko wake utaendelea kufadhili miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Tanzania ili nchi ifikie malengo yake ya kuwaletea wananchi maendeleo kupitia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
“Mradi huu wa kimkakati wa kusambaza nishati ya umeme kwa wananchi ni hatua muhimu kwa ajili ya kufikia malengo na matamanio ya wananchi ya kujiletea maendeleo lakini ni kielelezo pia cha ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Umoja wa Nchi za falme za Kiarabu ambao wameweka mipango ya kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa kuwa ni mdau mkuu wa maendeleo”, alisema Mhe. Suwaidi.
Alisema kuwa Mfuko huo utaendelea kuangalia fursa nyingine za ushirikiano katika nyanja mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana Tanzania ikiwemo sekta ya utalii, kilimo, ujenzi wa makazi ya kisasa kwa ajili ya watumishi katika Serikali ya Mapinduzi-Zanzibar, miundombinu ya barabara, kilimo pamoja na nishati.
Miongoni mwa miradi ambayo Mfuko huo umetoa fedha kwa Tanzania ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Wete-Pemba, barabara ya Kidawe hadi Uvinza (km 77), ujenzi wa Kiwanda cha Sukari Kagera na mradi wa maji Zanzibar vijijini ambayo imekamilika na hivi sasa wanafadhili ujenzi wa barabara ya Uvinza-Ilunde hadi Malagarasi wenye thamani ya dola za Marekani milioni 15.