Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), umewatoa hofu Watanzania kuhusu ubora wa vifaa vinavyotumika katika utekelezaji wa miradi inayoendelea nchini ikisema ni imara na bora.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, alitoa ufafanuzi huo jana mkoani Dodoma baada ya kufanya ziara ya ukaguzi katika maabara inayotumika kupima viwango na ubora wa vifaa.
Pia alifanya ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje wa Jiji la Dodoma sehemu ya pili, kutoka Nala-Veyula-Mtumba (Km 52.3) ambayo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 51.
Wakati wa ukaguzi huo, Mhandisi Besta, aliwataka wataalamu hao kuhakikisha kuwa vifaa vyote vya ujenzi ikiwemo nondo, kokoto, udongo vinapimwa kwa weledi kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa katika utekelezaji wa mradi.
"Serikali inatumia fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi yake, hivyo wataalam ambao mmeaminiwa kusimamia miradi hii pamoja na mshauri mwelekezi hakikisheni mnapima malighafi zote za ujenzi na endapo mtakuta hazikidhi vigezo visitumike katika mradi wowote," alisema Mhandisi Besta.
Aidha, Mhandisi Besta alisema katika kuhakikisha ubora na viwango vya ujenzi vinazingatiwa, wanaendelea kufuatilia upimaji wa malighafi zote zinazotumika katika miradi yote inayosimamiwa na TANROADS ili kuhakikisha barabara na madaraja yanayojengwa yanadumu na kukidhi thamani ya fedha.
“Miradi yote iliyopo chini ya TANROADS inafuatiliwa kwa umakini na ubora kulingana na thamani ya fedha ambayo imewekwa”, alisema Mhandisi Besta.
Naye Mhandisi wa vifaa, anayesimamia mradi wa barabara ya mzunguko wa nje jijini Dodoma, Mhandisi Deogratius Nyambo alisema kuwa vifaa vyote kabla havijaanza kutumika huingizwa katika maabara kwa ajili ya kupimwa ubora na endapo vitabainika havijakidhi huondolewa sehemu ya mradi.
Alisema katika kusimamia ubora kuna kazi za kila siku zinazofanyika ikiwemo kupima ubora wa udongo, tabaka la tuta la barabara kulingana na viwango vilivyowekwa vya mradi husika ili kuhakikisha barabara na madaraja vinadumu kwa muda mrefu.
Barabara ya mzunguko wa nje wa Jiji la Dodoma (Km 112.3) ambayo ujenzi wake umegawanywa katika sehemu mbili, ambazo ni Nala-Veyula-Mtumba (Km 52.3) pamoja na Ihumwa-Matumbulu-Nala(Km 60) unatarajiwa kukamilika Desemba mwakani, ambapo pamoja na mambo mengine itapunguza msongamano katika jijini Dodoma na kuchochea shughuli za kiuchumi.