Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TANESCO Changamkieni Fursa Muunganishe Wateja – Naibu Waziri
Jul 16, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Veronica Simba – Ulanga

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwa wabunifu na kuzitumia vema fursa za kibiashara zinazojitokeza kwa kupeleka umeme katika maeneo mbalimbali yenye wateja wengi wanaohitaji huduma hiyo.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Iputi, Kata ya Mbuga, wilayani Ulanga, Naibu Waziri alisisitizia kauli yake hiyo na kuwaagiza Meneja wa Kanda na Mkoa, kuandaa Mradi mdogo unaolenga kuwapelekea umeme wananchi wa eneo hilo mapema iwezekanavyo, kabla hawajafikiwa na Mradi wa Ujazilizi.

“Nawaachia kazi hii, muandae Mradi wa kuwaletea wananchi hawa umeme. Nimeona uwezo wa kulipa wanao na wamesubiri kwa muda mrefu sana. Wako tayari.”

Kabla ya kutoa agizo hilo, Naibu Waziri aliwauliza wananchi ikiwa wako tayari kupelekewa huduma hiyo na TANESCO kwa gharama ya shilingi 177,000 au wasubiri Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA IIIA) uwafikie ambao utawagharimu shilingi 27,000 tu; ambapo kwa umoja wao walitaka wapelekewe umeme wa TANESCO kwa madai kuwa wanao uwezo wa kulipia.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alikiri kukerwa na utendaji kazi duni uliooneshwa na Mkandarasi MBH, aliyekuwa akitekeleza Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II) katika Mikoa ya Pwani na Morogoro; ambapo alieleza kwamba ndiyo sababu Serikali haijampatia tena kazi.

Kufuatia suala hilo, Naibu Waziri aliwaagiza watendaji husika wa TANESCO, kuandaa Taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo na kuiwasilisha ofisini kwake Dodoma, kabla ya Ijumaa ijayo, Julai 20 mwaka huu.

“Natambua kuwa Mkandarasi husika alikwishalipwa lakini zipo fedha kidogo zilizosalia kukamilisha malipo yake. Tutafute utaratibu utakaowezesha kuhamishia fedha hizo TANESCO ili zisaidie kutekeleza Mradi wa Ujazilizi badala ya kumlipa mtu ambaye ametutia hasara kwa utendaji duni,” alisisitiza.

Naibu Waziri pia, alitoa onyo kwa wakandarasi wanaotekeleza Miradi mbalimbali ya Umeme Vijijini, hususan REA III, kuwa Serikali haitamvumilia yeyote atakayeharibu kazi kwa namna yoyote.

Aidha, sambamba na onyo hilo, alisema kuwa, Serikali itamuwajibisha pia Msimamizi wa Serikali wa Mradi husika, ambaye atabainika kushindwa kumsimamia ipasavyo Mkandarasi na kusababisha kutotekelezwa kwa Mradi kikamilifu.

Maelekezo mengine aliyoyatoa Naibu Waziri katika ziara hiyo, ni kwa TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kuhakikisha wanaunganisha umeme katika maeneo yote yaliyopitiwa na miundombinu ya umeme.

Akifafanua zaidi, alisema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano haitaki kuona wananchi ambao wamepitiwa na miundombinu ya umeme, wakiishia kuangalia tu nyaya na nguzo pamoja na kuzilinda huku wao wenyewe wakiwa hawana umeme.

“Hili ni agizo kutoka kwa viongozi wetu wa juu, wakiongozwa na Mheshimiwa Rais John Magufuli, hivyo kilichobaki ni utekelezaji wake.”

Naibu Waziri amekuwa katika ziara ya kazi kwa takribani wiki tatu, katika mikoa mbalimbali nchini, kukagua utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya umeme pamoja na kuzungumza na wananchi. Vijiji vingine alivyotembelea wilayani Ulanga, ambako ndiko amehitimisha ziara yake, ni pamoja na Chikwera, Kata ya Mwaya pamoja na Kijiji cha Makanga, Kata ya Vigoi.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi