Imeelezwa kuwa Tamasha la Kizimkazi kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi wa Wilaya ya Kusini Unguja kutokana na shughuli mbalimbali zinazofanyika katika tamasha hilo ikiwemo uzinduzi wa miradi.
Hayo yameelezwa na Afisa Utamaduni wa Wilaya ya Kusini, Othman Abdallah wakati wa mahojiano maalum na Ofisi ya Idara ya Habari-MAELEZO, Paje mkoani Unguja Kusini.
“Tamasha hili la Kizimkazi ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi katika wilaya yetu, hii inatokana na uzinduzi wa miradi mbalimbali katika tamasha hili, ambapo kwa mwaka huu miradi inayoenda kuzinduliwa ni pamoja na hoteli yenye hadhi tano iliyopo katika Kata ya Paje pamoja na tawi jipya la NMB lilipo Paje,” amesema Othman.
Othman ameeleza historia ya tamasha hilo, kuwa lilianza wakati Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipochaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania Bara, ambapo mara baada ya kuchaguliwa alienda kuwaaga wapiga kura wake katika Kata ya Kizimkazi ndipo wananchi wa eneo hilo walipoamua kuwa na siku ya Mhe. Samia ambayo waliita Kizimkazi.
“Tamasha la Kizimkazi limendelea kukua siku hadi siku, na kwa mwaka huu tamasha hili limechukua sura ya kiwalaya na si eneo la Kizimkazi peke yake,” amesema Othman.
Aliendelea kusema, nia kubwa ya kuanzishwa kwa tamasha hilo ni kudumisha mila na desturi ya wakazi wa Kizimkazi, lakini kwa sasa tamasha hilo limekuwa zaidi ambapo kwa mwaka huu limeadhimishwa katika ngazi ya wilaya.
“Nia ya Mhe. Rais Dkt. Samia ni tamasha hili kuendelea kukua mpaka kufikia ngazi ya kimataifa, ili lichochee uchumi pamoja na kutangaza utalii wa nchi kupitia tamasha hilo,” amesema Othman.