Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tamasha la Kizimkazi Kuchochea Utalii Zanzibar - Dkt. Mwinyi
Aug 26, 2023
Tamasha la Kizimkazi Kuchochea Utalii Zanzibar - Dkt. Mwinyi
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akitoa hutuba yake ya uzinduzi wa Tamasha la Kizimkazi (KIZIMKAZI DAY) lililofanyika viwanja vya Kashangae Paje, Wilaya ya Kusini.
Na Lilian Lundo - Paje, Zanzibar

Tamasha la Kizimkazi lililoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, likiwa na lengo la kudumisha mila na desturi ya Wananchi wa Kizimkazi limetajwa kuwa kichocheo kikubwa cha utalii Mkoa wa Kusini Unguja.

Tamasha hilo kwa mwaka huu 2023 linafanyika Paje mkoani Kusini Unguja kuanzia Agosti 26 hadi 31, 2023 ambapo limefunguliwa leo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi.

“Nampongeza Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuasisi Tamasha la Kizimkazi ili kudumisha mila na desturi ya Wananchi wa Kizimkazi,” amesema Mhe. Dkt. Mwinyi.

Aidha amesema kuwa, tamasha hilo ni njia mojawapo ya kudumisha utamaduni wa Mtanzania, ambapo huenda sambamba na ubunifu wa maeneo mbalimbali ya utalii wa ndani.

Ameendelea kusema kuwa, tamasha hilo linatoa fursa ya ajira, kuvutia watalii pamoja na kuimarisha utalii wa ndani.

“Ni matumaini yangu kuwa, katika miaka ijayo tamasha hili litakuwa kivutio kikubwa cha watalii,” amesema Mhe. Dkt. Mwinyi.

Aidha, ametoa wito kwa uongozi wa mkoa kutumia tamasha hilo kutangaza maeneo mbalimbali ya uwekezaji yaliyomo mkoani humu.

Vilevile amewashukuru wawekezaji kwa kuchangia Pato la Taifa, kuongeza idadi ya watalii pamoja na kutoa ajira kwa wananchi.

“Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji na kufungua milango ya uwekezaji zaidi,” amesema Mhe. Dkt. Mwinyi.

Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa tamasha hilo katika kilele cha tamasha hilo Agosti  31, 2023 ambapo atafungua miradi mbalimbali mkoani humo pamoja na kutoa misaada kwa wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 80 na watoto yatima.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi