Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tamasha la Busara Kuenzi Sanaa na Utamaduni wa Mwafrika
Jan 22, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu.

Watanzania wametakiwa kuenzi sanaa na utamaduni walionao kwa ajili ya kizazi kijacho ili kukijengea uzalendo wa kupenda nchi yao.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Yusuf Mahmoud wakati akielezea ujio wa Tamasha la 15 linalotarajiwa kufanyika Ngome Kongwe, Unguja - Zanzibar na kushirikisha wanamuziki na vikundi mbali mbali vya sanaa kutoka pande zote za bara  la Afrika na Ulaya.

“Katika Tamasha hili, ni sehemu ambapo watu wenye weledi wa sanaa mbalimbali hukutana, kuanzia kwa wakurugenzi wa matamasha mpaka kwa wazalishaji wa muziki, mameneja wa wanamuziki, wasambazaji wa muziki, wote hawa huja hapa Zanzibar mwezi Februari kuja kushuhudia utamu wa midundo ya muziki wa Ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Mahmoud.

Anaongeza kuwa, “Hili siyo tu tukio ambalo watumbuizaji wa Tamasha pekee huhudhuria, bali hata baadhi ya wanamuziki ambao hawapo katika orodha ya kutumbuiza huja kwa minajili ya kujifunza kutoka kwa wale wanaofanya maonesho mbalimbali, na pia hupata fursa ya kufahamiana na wadau muhimu wa tasnia yao na kutengeneza mahusiano ya kikazi kwa miezi ijayo, hata zaidi ya hapo baada ya tamasha kuisha.”

Likisifika kuwa miongoni mwa matamasha yanayoheshimika, Sauti za Busara likiwa na kauli mbiu ya “Kuunganishwa na Muziki” kwa mwaka huu, linawakutanisha pamoja zaidi ya wanamuziki 460 katika visiwa vya Zanzibar.

Likiwa ni tamasha ambalo limeshuhudia ukuaji mkubwa katika uadhimishwaji wake na mwaka huu ukiwa wa 15, Tamasha hili linavutia wataalamu wa habari na muziki kutoka katika kila pembe ya Afrika, Ulaya na mahali pengine, ambapo hutoa jukwaa la kipekee kwa wanamuziki wa Afrika Mashariki kuutanganza muziki wao duniani.

“Kila mwaka, kila mwanamuziki anayepata fursa ya kutumbuiza katika jukwaa la Sauti za Busara, hualikwa kuzunguka katika miji mbalimbali duniani na kufanya maonesho kwenye matamasha yanayofanyika katika nchi hizo. Wanamuziki ambao hupata fursa ya kualikwa aghalabu, ni wale ambao wamethibitika katika maonesho yao kuwa wabunifu, wenye kuzungumza ujumbe fulani, na wanaocheza muziki wenye utambulisho fulani,” anasema Yusuf, akiwataja Msafiri Zawose, Jagwa Music, Leo Mkanyia, Tausi Women’s Taarab na Maulidi ya Homu ya Mtendeni kama mifano ya vikundi vya Kitanzania ambavyo tayari vimekwishaitwa katika safari za kimataifa baada ya kuonekana katika Tamasha la Sauti za Busara.

Kulingana na maelezo ya Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Yusuf  Mahmoud, Tamasha la Sauti za Busara ni fursa adhimu ambayo wanamuziki kutoka Tanzania hawatakiwi kukosa, kwa kuwa fursa kama hizi ni chache na ngumu kuzipata ndani ya Afrika.

“Watu wa rangi tofauti huungana kwa pamoja kusheherekea muziki wa Kiafrika. Matarajio na msisimko ni mkubwa, hoteli zinazopatikana Stone Town huwa zinajaa katika wiki ya tamasha zikiwahudumia watu wanaotoka katika kila kona ya Tanzania, Afrika na Ulaya,” anasema Yusuf.

Kwa makadirio ya haraka, tamasha linachangia kiasi cha Dola za Marekani 7 milioni katika uchumi kila mwaka, kikiwa ni kipindi cha mavuno kwa biashara nyingi zinazofanyika kwenye kila pembe ya Zanzibar na sehemu zingine, na kulifanya Tamasha la Sauti za Busara kuwa zaidi ya ‘Tamasha la Muziki’.

Hata hivyo, licha ya kuwa na mafanikio hayo yote, lakini changamoto kubwa inayolikumba tamasha hili ni ufadhili, na ndiyo sababu hata tamasha la mwaka 2016 lilifutwa na kusababisha hasara kubwa sana kwa biashara nyingi visiwani Zanzibar.

“Tunaendelea kutegemea fedha za wafadhili kutoka katika balozi mbalimbali, ambapo balozi za Norway na Uswisi zikiwa miongoni mwa wafadhili wakubwa, zikisaidia mafunzo na jitihada za ujengaji uwezo,” anasema Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Yusuf Mahmoud.

Tamasha la Sauti za Busara 2018 linafadhiliwa na Ubalozi wa Norway, Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na Zambia, Africalia, Mozeti, Zanlink, Memories of Zanzibar, Zenj FM, Chuchu FM, Tifu TV, Music In Africa, Ikala Zanzibar Stone Town Lodge, Emerson Zanzibar, Coastal Aviation, 2Tech Security, Ubalozi wa Ujerumani, Golden Tulip Dar City Centre.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi