Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametekeleza ahadi ya shilingi milioni 500 aliyoitoa kwa Timu ya Taifa Stars ikifuzu kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2023 nchini Ivory Coast.
Akizungumza na wachezaji na viongozi wa timu hiyo Septemba 7, 2023 nchini Algeria, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Saidi Yakubu ambaye aliongoza msafara wa timu hiyo, amewapongeza wachezaji na benchi la ufundi kwa kazi kubwa waliyofanya kwa kuwa safari ya matokeo hayo haikuwa nyepesi hadi dakika ya mwisho.
“Kwa niaba ya Serikali Mhe. Rais, Mhe. Waziri pamoja na wadau wote, tumekuja hapa kuongeza hamasa. Kubwa mtakumbuka wakati wa kujiandaa na mechi ya Uganda kule nyumbani, Mhe. Rais alitoa ahadi ya kutoa shilingi milioni 500, timu ikifuzu. Nafurahi kuwaambia kwamba hizo fedha sio tu kwamba zitatolewa, zimekwisha letwa Wizarani kwa ajili yenu”, amesisitiza Katibu Mkuu, Bw. Yakubu.
Timu ya Tanzania, Taifa Stars imefuzu kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) baada ya kutoka sare ya bila kufungana (0-0) na Algeria katika mchezo wa mwisho wa Kundi F uliochezwa katika Uwanja wa May 19, nchini Algeria.
Taifa Stars ikiwa na alama 8 imeungana na Algeria yenye alama 16 katika kundi hilo kushiriki mashindano ya AFCON yatakayofanyika Ivory Coast na kuziacha nje ya mashindano hayo timu za Uganda waliomaliaza na alama 7 na Niger waliomaliza na alama 2 huku Tanzania ikishiriki mashindano ya AFCON kwa mara ya tatu kihistoria baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria na 2019 nchini Misri.