Na.Jacquiline Mrisho.
Chama cha Wamiliki wa Mabasi Yaendayo Mikoani (TABOA) na Umoja wa Wasafirishaji Abiria Jijini Dar es Salaam (UWADAR) wamekanusha taarifa inayosambazwa kwenye mitandao kuwa Novemba 14 mwaka huu watakuwa na mgomo wa kusitisha huduma za usafirishaji.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa UWADAR, Kismat Dhalla wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kwa ajili ya kukanusha suala hilo.
Dhalla amesema kuwa taarifa hiyo iliandaliwa na vyama hivyo lakini ilishatolewa katika vyombo vya habari siku nyingi zilizopita hivyo kuna baadhi ya watu wameamua kuisambaza upya bila ridhaa ya wahusika.
“Ni kweli ile taarifa ni ya kwetu lakini tulishaitoa siku nyingi na mgomo huo haukufanyika kwa kuwa tuliahidiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) kuwa itayafanyia kazi madai yetu”, alisema Dhalla.
Dhalla ameongeza kuwa tayari SUMATRA imeandaa mkutano na wadau ambao utafanyika mnamo Novemba 15 mwaka huu kwa ajili ya kujadili kuhusiana na baadhi ya Kanuni zilizotungwa katika Sheria hiyo ya SUMATRA.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa SUMATRA, Tumaini Silaa amesema kuwa lengo la SUMATRA ni kuhakikisha kuwa usafiri unapatikana muda wote na unamfaidisha msafiri na msafirishaji ndio maana mamlaka hiyo inajitahidi kuyamaliza malalamiko ya TABOA na UWADAR pindi yanapojitokeza.
“Sisi kama SUMATRA tunaona kuwa hakuna mgogoro kati yetu na wadau wa usafiri isipokuwa ni kutoelewa Kanuni ambazo zimepitishwa na Mhe. Waziri mwenye dhamana hivyo tutakapokutana katika mkutano huo tutaeleweshana kwani tunaamini kuwa kanuni zilizoandaliwa ziko vizuri”, alisema Bw.Silaa.
Amefafanua kuwa baadhi ya watu bado wanachanganya Kanuni za mwaka 2007 ambazo zimefutwa na kanuni hizi mpya lakini wanatakiwa kufahamu kuwa kanuni mpya zimeweka usawa kwa upande wa msafirishaji, abiria, dereva na kondakta.
Pia, kanuni hizo mpya bado hazijaanza kutumika mpaka pale SUMATRA itakapotoa elimu ili kila mmoja awe na uelewa na Sheria na Kanuni zake.