Na Jacquiline Mrisho
Taasisi za Umma zimeshauriwa kuwa na akaunti za makusanyo kwenye benki zaidi ya moja kati ya benki zilizoungwa na Mfumo wa Serikali wa Ulipaji wa Kielektroniki (GePG) ili kuwarahisishia walipaji wa huduma za serikali.
Ushauri huo umetolewa leo jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu wakati akifungua mkutano wa mwaka wa watumiaji wa mfumo wa GePG katika ukusanyaji wa fedha za umma uliozishirikisha taasisi za Umma zinazotumia Mfumo huo pamoja na timu ya GePG kwa ajili ya kujengeana uwezo wa namna bora ya kutumia mfumo huo.
Dkt. Kazungu amesema kuwa utaratibu wa malipo kupitia GePG unatoa fursa ya kuwa na njia nyingi za kulipia fedha za umma pamoja na kuwapa walipaji wa huduma za serikali utaratibu rafiki na machaguo mengi ya kufanya malipo.
"Kwa kuwa malipo yote yanayopitia GePG hayatozwi ada za miamala na benki hizo hivyo kuongeza akaunti za makusanyo katika benki hakutoongeza gharama za miamala kwa taasisi za umma bali kufanya hivyo kutaondoa hatari ya Ofisi husika kukosa huduma ya malipo endapo benki inayotumika itashindwa kutoa huduma kwa sababu mbalimbali", alisema Dkt. Kazungu.
Dkt. Kazungu ameongeza kuwa utaratibu huo wa makusanyo kupitia GePG unaenda sambamba na utekelezaji wa maelekezo mengine ya Serikali yanayohusu makusanyo ikiwemo yale yanayotaka akaunti kuu za makusanyo za taasisi za umma kuwepo benki kuu ya Tanzania (BoT).
Aidha, Naibu Katibu Mkuu amezitaja baadhi ya faida za mfumo huo zikiwezo za kuongezeka kwa uwazi na udhibiti katika ukusanyaji wa fedha za umma, kupata taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu makusanyo pamoja na kuwa na viwango na utaratibu unaofanana katika ukusanyaji wa fedha za umma kwa taasisi zote za umma.
Vile vile, mfumo huo unachochea ubunifu katika ukusanyaji wa pesa za Serikali na sekta ya fedha kwa ujumla kwa kuweka mazingira rafiki na ya usawa kwa wakusanyaji, kutoa huduma bora na rahisi ya malipo ya fedha za umma pamoja na kusaidia fedha kufika haraka katika akaunti kuu za makusanyo za taasisi.
Amezikumbusha taasisi ambazo bado hazijajiunga na mfumo wa GePG kuwa ifikapo Juni 30 mwaka 2019 hakutokuwa na fedha yoyote ya umma itakayokusanywa nje ya mfumo huo, hivyo wakati wa kujiunga na kuunganisha mifumo yao na mfumo huo ni sasa.
Mnamo Juni 2017, Serikali iliifanyia marekebisho sheria ya Fedha za Umma (PFA) ya mwaka 2001 na kuiongezea kipengele kinachotaka fedha zote za umma zikusanywe kupitia Mfumo wa Government e-Payment Gateway (GePG), hadi sasa jumla ya Benki 11 na mitandao sita ya malipo kwa njia ya simu za kiganjani zimeunganishwa na mfumo huo.