Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Jul 04, 2017
Na Msemaji Mkuu

Serikali ya Sudan Kusini imeoimba Tanzania kuisaidia katika utoaji wa mafunzo mbalimbali kwa wataalamu wake hasa wa sekta ya afya, kilimo na kupatiwa walimu wa lugha la Kiswahili kwa sababu taifa hilo linataka kuanza kufundisha lugha hiyo kwenye shule mbalimbali nchini humo.

Makamu wa Kwanza Rais wa Serikali ya Sudan Kusini Jenerali Taban Deng Gai ametoa maombi hao baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe Samia Suluhu Hassan kando mwa Mkutano 29 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika Jijini Addis Ababa Ethiopia.

Jenerali Taban Deng ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Sudan Kusini kupitia Jumuiya mbalimbali hususan Jumuiya ya Afrika Mashariki katika juhudi zake za kutafuta amani ya kudumu pamoja na kuwavumilia kadri inavyowezekana hasa wanapopitia changamoto mbalimbali kufikia amani hiyo.

Makamu huyo wa Kwanza Rais wa Serikali ya Sudan Kusini amemweleza Makamu wa Rais kuwa Serikali ya Tanzania ni mdau muhimu wa maendeleo kwa taifa hilo changa barani Afrika hivyo kuna umuhimu mkubwa kwa Serikali ya Tanzania kuendelea kulisaidia taifa hiyo ili liweze kuimarisha hali ya ulinzi na usalama pamoja na uimarishaji wa utoaji wa huduma za msingi kwa wananchi wake.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameihakikishia Serikali ya Sudani kuwa Tanzania itakuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kijamii ikiwemo juhudi za uimarishaji wa hali ya ulinzi na usalama katika taifa hilo.

Makamu wa Rais amesema ili Tanzania iweze kushirikiana vizuri na Serikali ya Sudan Kusini ni muhimu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiriano wa Kimataifa  za nchi hizo Mbili kuandaa mfumo maalum wa ushirikiano na utekelezaji wake ambao utaanisha maeneo  ya kushirikiana katika sekta mbalimbali kutokana na taifa hilo changa barani afrika kuwa na changamoto nyingi hasa kwenye sekta za afya, elimu, kilimo, siasa, ulinzi na usalama.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan katika mazungumzo hayo  ameziomba Wizara za Mambo ya Nje za nchi zote Mbili kuandaa mpango huo haraka kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa pande hizo Mbili.

Makamu wa Rais pia ameonyesha kuguswa sana na tatizo na vifo vinavyatokana na uzazi na ameshauri Serikali ya Sudan Kusini, pamoja na changamoto zao za kiuchumi ijaribu kuboresha kadri itakavyoweza, miundombinu ya barabara, magari ya kusafirisha wangonjwa kwa haraka, vifaa tiba na kuimarisha vyumba vya dharura vya uzazi ili kukabiliana na tatizo hilo.

Kuhusu tatizo la uhaba wa chakula, Makamu wa Rais aliguswa pia na changamoto hiyo inayoendelea kuikumba Sudan Kusini na ameridhika kusikia kuwa kuna jitihada zilifanywa na Serikali yao kuja Tanzania kwa ajili ya kutafuta chakula cha kutosha kwa ajili ya wananchi wake.

Makamu wa Rais pia amepongeza jitihada zinachukuliwa na Serikali ya Sudan Kusini chini Rais wao Salva Kiir ya kutafuta suluhu mgogoro wa kisiasa nchi humo.

Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Mauritius Anerood Jugnauth Jijini Addis Ababa – Ethiopia na ametumia sehemu ya mazungumzo hayo kuwakabirisha wawekezaji kutoka taifa hilo kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania itaendelea kudumisha na kuendeleza mahusiano yaliyopo kati ya Mataifa hayo Mawili na Tanzania itaendelea kujifunza zaidi kutoka kwa nchi ya Mauritius hasa namna ya kuimarisha shughuli za utalii na namna bora ya kuongeza uzalishaji wa Sukari ili kukabiliana na uhaba wa bidhaa hiyo.

Makamu wa Rais pia amesisitiza uharakishaji wa kusainiwa kwa mikataba ya makubaliano kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa pande hizo Mbili.

Naye, Waziri Mkuu wa Mauritius Anerood Jugnauth amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa taifa hilo litaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali kwa ajili ya maslahi ya wananchi wa nchi hizo Mbili.

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais wa

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

ADDIS ABABA- ETHIOPIA.

4-Julai-2017.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi