Kuhusu Walioteuliwa Kugombea Udiwani Katika Kata 43 Zitakazofanya Uchaguzi Mdogo Tarehe 26 Novemba, 2017
Tarehe 26 Oktoba, 2017, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilifanya Uteuzi wa Wagombea Udiwani kwa ajili ya Uchaguzi Mdogo katika Kata 43 zilizopo kwenye Halmashauri 36 za Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika tarehe 26 Novemba, 2017.
Jumla ya Wanachama Wagombea 177 wa vyama mbalimbali walichukua Fomu ya Uteuzi Na. 8C na Fomu ya Maadili ya Uchaguzi Na. 10, kati yao 174 sawa na asilimia 92.7 ni wanaume na 13 sawa na asilimia 7.3 ni wanawake.
Jumla ya Wanachama 155 sawa na asilimia 87.6 ya waliochukua fomu za Uteuzi walizirejesha na kuteuliwa kuwa Wagombea ambapo 145 sawa na asilimia 93.6 ni Wanaume na Wagombea 10 sawa na asilimia 6.4 ni Wanawake.
Hadi muda wa mwisho wa Uteuzi ulipofika saa 10.00 jioni jumla ya Wanachama 22 sawa na asilimia 12.4 ya waliochukua fomu hawakuteuliwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutorudisha fomu, kurudisha fomu nje ya muda uliotakiwa kisheria na fomu kutojazwa ipasavyo.
Vyama 13 vimesimamisha Wagombea na idadi ya Kata kwa kila Chama ni kama ifuatavyo: ACT-Wazalendo Wagombea 18 (sawa na asilimia 40), ADA-TADEA Mgombea 1 (sawa na asilimia 2), ADC Wagombea 4 (sawa na asilimia 7), CCM Wagombea 43 (sawa na asilimia 100) CHADEMA Wagombea 42 (sawa na asilimia 98), CHAUMA Mgombea 1 (sawa na asilimia 2), CUF Wagombea 30 (sawa na asilimia 70), DP Wagombea 3 (sawa na asilimia 5), NCCR-MAGEUZI Wagombea 6 (sawa na asilimia 16), NRA Wagombea 2 (sawa na asilimia 5), SAU Wagombea 2 (sawa na asilimia 5), TLP Mgombea 1 (sawa na asilimia 2) na UDP asilimia 2 (sawa na asilimia 5).
Aidha jumla ya Wagombea 30 sawa na asilimia 19.4 ya Wagombea walioteuliwa waliwekewa pingamizi na Wagombea wenzao na Msajili wa Vyama vya Siasa kutokana na sababu mbalimbali.
Kwa mujibu wa Ratiba ya Uchaguzi Kampeni za Uchaguzi tayari zimeanza na zitaendelea hadi tarehe 25 Novemba, 2017 ikiwa ni siku moja kabla ya Siku ya Uchaguzi.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inavikumbusha Vyama vya Siasa na Wagombea wao kuwa vinapaswa kuzingatia Maadili ya Uchaguzi wa Rais Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015 wakati wote wa Kampeni na hata Siku ya Uchaguzi.
Taarifa zaidi kuhusu walioteuliwa na vyama vyao inapatikana kwenye tovuti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.www.nec.go.tz na NEC ONLINE TV-TANZANIA.
Imetolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi tarehe 31 Oktoba, 2017.