Ukaguzi Bandarini Hauna Lengo la Kuwabagua Wazanzibari
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ukaguzi unaofanywa kwenye bandari ya Dar es Salaam kwa wasafiri wanaokwenda Zanzibar, hauna lengo la kuwabagua bali ni kuimarisha ulinzi wa mipaka ya nchi.
“Hatulengi kuzuia biashara za wafanyabiashara ndogondogo, bali tunaimarisha ukaguzi ili kuzuia wasafirishaji wa dawa za kulevya, wasambazaji na wauzaji,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Alhamisi, Aprili 19, 2018) Bungeni mjini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Bw. Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kupata kauli ya Serikali juu ya kuwapunguzia makali wafanyabiashara wanaotoka Zanzibar.
Waziri Mkuu amesema: “Wanaofanya ukaguzi pale bandarini siyo watu wa TRA peke yao kama Mheshimiwa Jaku alivyosema, bali tukumbuke kuwa Tanzania imeingia katika vita ya dawa za kulevya, kwa hiyo tunaimarisha ulinzi wa mipaka yetu.”
“Tanzania inapambana na matumizi ya dawa za kulevya, kwa hiyo ukaguzi huu umelenga kuzuia watumiaji, wasambazaji na wasafirishaji wa dawa hizo. Upekuzi huu umelenga kupunguza hili tatizo, umelenga abiria wote na siyo Wazanzibari peke yao,” amesisitiza.
Amesema Serikali inaendelea na mipango ya kutafuta mitambo ya kisasa ya kukagua mizigo ya wasafiri wanaotumia bandari za Tanzania bara.
Mapema, akiuliza swali lake, Mhe. Jaku alisema: “Kilio cha wabunge wengi wanaotoka Zanzibar hapa Bungeni ni bandari ya Dar es Salaam kutoza kodi wafanyabiashara wadogo wanaosafirisha TV au vyerehani. Ni lini utakaa nao au kufanya ziara ya kushtukiza ili ujionee hali halisi?”
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, APRILI 19, 2018.