Rais Magufuli aagiza usajili wa meli mpya usitishwe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar Balozi Ali Abeid Karume kusitisha usajili wa meli mpya hapa nchini mpaka hapo itakapotangazwa vinginevyo.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 19 Januari, 2018 alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, kikao ambacho kimehudhuriwa na Mawaziri hao.
Ametoa agizo hilo ili kujipanga upya kufuatia taarifa za kukamatwa kwa dawa za kulevya katika meli zinazopeperusha bendera ya Tanzania ambazo hadi sasa zimefikia meli 5.
Sambamba na kusitishwa kwa usajili mpya wa meli Mhe. Rais Magufuli amewaagiza Mawaziri hao pamoja na vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina kwa meli zote 470 ambazo zimesajiliwa hapa nchini na zinapeperusha bendera ya Tanzania.
Pia Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Augustine Mahiga kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo na kuhakikisha jina la Tanzania halichafuliwi ndani na nje na nchi.
“Kafanyeni uchunguzi wa kina kwa meli zote zinazopeperusha bendera ya Tanzania, fanyeni uchunguzi kwa meli zilizokamatwa ambazo ni 5 na pia hizi 470 zilizosajiliwa na zinazoendelea kufanya kazi zichunguzeni, hatuwezi kuacha jina la nchi yetu lichafuliwe na watu wanaofanya mambo kwa maslahi yao” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametaka maagizo yote yaliyotolewa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kuhusiana na meli hizo yatekelezwe.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amewataka wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutilia mkazo utekelezaji wa sera ya diplomasia ya uchumi ili nchi iweze kunufaika na fursa mbalimbali za uhusiano na ushirikiano na mataifa mengine duniani.
Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri Mahiga kuhakikisha Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi, na Wakurugenzi wa idara za wizara hiyo wanafanya kazi zenye manufaa kwa nchi, ikiwemo kuwataka Mabalozi kutoa taarifa kila baada ya robo mwaka juu ya ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa sera hiyo.
“Wakupe taarifa kila baada ya robo mwaka, na Balozi ambaye atakuwa hakusanyi mapato vizuri na kuinua biashara na uwekezaji atakuwa hafai kuendelea kuwa Balozi, tena kawaambie kabisa kwenye suala hili hakuna mchezo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amemtaka Waziri Mahiga na watendaji wa wizara yake kufuatilia kwa ukaribu na kushirikiana na Mawaziri wanaohusika katika utekelezaji wa mikataba mbalimbali ambayo Tanzania imetiliana saini na nchi mbalimbali duniani, na kwamba hataki kusikia utekelezaji wa mikataba ambayo baadhi yake inahusisha miradi mikubwa yenye manufaa kwa Tanzania, unakwama ama kusuasua.
“Mnapokuwa mnahitaji taarifa kutoka wizara nyingine kama ni Waziri muandikie Waziri mwenzako kama ni Katibu Mkuu muandikie Katibu Mkuu mwenzako halafu nakala ya barua ilete kwangu kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, nataka nione huyo atakayechelewesha ama kutotoa taarifa” ameongeza Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
19 Januari, 2018