Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma.
Jan 19, 2018
Na Msemaji Mkuu

WAZIRI MKUU AKABIDHI KADI ZA MATIBABU KWA WAZEE 280

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amegawa kadi za matibabu kwa wazee 280 wa wilaya ya Serengeti mkoani Mara, kadi hizo zitawawezesha wazee hao kutibiwa bure.

Amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kutoa matibabu bure kwa wazee walio na umri wa kuanzia miaka 60.

Waziri Mkuu alikabidhi kadi hizo jana (Alhamisi, Januari 18, 2018) alipotembelea mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Serengeti, inayojengwa katika mji wa Mugumu.

Alisema Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Serengeti itakamilisha ujenzi wa hospitali hiyo, itakayokuwa na uwezo wa kuwahudumia wakazi wa wilaya hiyo na wageni.

Waziri Mkuu alisema ujenzi wa hospitali hiyo ni muhimu kwa kuwa mbali na kuwanufaisha wananchi, pia watalii wanaotembelea mbuga ya Serengeti nao wataweza kutibiwa hapo.

Awali, Mkuu wa wilaya hiyo Bw. Nurdin Babu alisema tangu mwaka 1974 wilaya hiyo ilipoanzishwa hadi sasa haina hospitali ya wilaya na wakazi wake wanatibiwa katika hospitali teule ya Nyerere inayomilikiwa na kanisa la Mennonite Tanzania.

Alisema kutokana na kuongeka kwa idadi ya wakazi hao pamoja na idadi kubwa ya wageni wanaotembelea Serengeti, hususan watalii hospitali hiyo haina tena uwezo wa kutoa huduma kwa kiwango kinachostahili.

Bw. Babu alisema mara nyingi wageni wanaotembelea mbuga ya Serengeti hulazimika kufuata huduma za afya mjini Arusha au Nairobi nchini Kenya pale wanapougua au kupata ajali katika shughuli zao za kitalii.

Alisema kwa upande wa wakazi wa wilaya ya Serengeti wao hulazimika kufuata huduma za afya katika hospitali ya Mkoa au hospitali ya Rufaa ya Bugando, hivyo kukamilika kwa mradi huo wa ujenzi wa hospitali utawapunguzia kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo.

Pia Mkuu huyo wa wilaya alisema alianzisha kampeni ya changia sh. 1,000 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya, kwa lengo la kuwafanya wakazi hao wajisikie kuwa wameshiriki katika ujenzi huo.

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU

IJUMAA, JANUARI 19, 2018.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi