WAZIRI MKUU AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA DARAJA MTO MARA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa mradi wa Daraja la Mto Mara katika barabara ya Tarime-Mugumu unaogharimu sh. bilioni 6.803.
Ameweka jiwe hilo la msingi leo (Alhamisi, Januari 18, 2018) baada ya kuwasili wilayani Serengeti kwa ziara ya kikazi akitokea wilayani Tarime mkoani Mara.
Mkataba wa ujenzi wa daraja hilo ulitiwa saini Februari 23, 2017 na kazi ilianza rasmi Machi 2, 2017 na linatarajiwa kukamilika Machi, 2018.
Amesema lengo la Serikali ni kuziunganisha wilaya hizo kwa barabara ya lami na wameanza na ujenzi daraja hilo.
Waziri Mkuu amesema kuwa daraja hilo litakuwa na barabara za maungio zenye urefu wa mita 900 kila upande na upana wa mita 6.5 na mabega ya mita 1.5 kila upande.
Kukamilika kwa daraja hilo kutafungua fursa za kibiashara na kiuchumi kati ya wilaya hizo za Tarime na Serengeti pamoja na nchi jirani ya Kenya.
Awali, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Mlima Ngaile alisema daraja hilo linajengwa na makapuni mawili ya kizalendo.
Alisema daraja hilo lina urefu wa mita 94 na upana wa mita 9.9, ambapo sehemu ya kupita magari ni mita 7.5 na watembea kwa miguu mita 1.175 kwa kila upande.
Mhandisi huyo alisema kwa muda mrefu mawasiliano ya wakazi wa Tarime na Serengeti pamoja na Kenya kibiashara na kiuchumi yamekua ya shida kwa kutokuwa na daraja imara.
“Daraja la chuma na mbao lililopo kwa sasa halina uwezo wa kupitisha magari makubwa yanayobeba mazao ya biashara kwa sababu uwezo wake ni kubeba tani 10 tu.”
Alisema kukamilika kwa daraja hilo lenye uwezo wa kubeba tani 56 litakuwa ni suluhu ya matatizo hayo na litaongeza kasi ya utoaji wa huduma za maendeleo kwa jamii inayozunguka wilaya za Tarime na Serengeti.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
ALHAMISI, JANUARI 18, 2018.