UKAGUZI WA KINGA NA TAHADHARI DHIDI YA MOTO
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeundwa na linatekeleza majukumu yake chini ya Sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji namba 14 ya mwaka 2007 (Fire and Rescue Force Act No. 14 of 2007). Majukumu makubwa ya Jeshi hili ni kuokoa Maisha na Mali katika majanga yatokanayo na moto, mafuriko, tetemeko la ardhi, ajali za barabarani pamoja na majanga mengine.
Sambamba na majukumu hayo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linafanya ukaguzi kwenye vyombo vya usafiri na usafirishaji, na kutoa ushauri uwekaji wa vifaa vya kinga na tahadhari. Ukaguzi huu unafanyika kwa mujibu wa sheria namba 14 ya mwaka 2007 ikisomwa pamoja na kanuni ya Vyeti na Usalama wa moto Mwaka 2008 na marekebisho ya mwaka 2014 (Fire and Rescue Force Safety Inspections and Certificates Regulations of 2008 GN.106 and its Amendment GN 63 of 2014.) Pamoja na kanuni ya tahadhari dhidi ya moto kwenye majengo ya mwaka 2015 (Fire and Rescue Force Fire Safety Precaution in Building Regulations of 2015 GN 516.)
Kwa kuzingatia majukumu hayo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linajulisha umma kuwa, halifanyi biashara ya kuuza vifaa vya kuzimia moto wala kuvifanyia matengenezo (service) vifaa hivyo pamoja na mifumo ya kinga na tahadhari dhidi ya moto. Bali Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linasimamia na kuhakiki ufungwaji wa vifaa hivyo.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatoa rai kwa wamiliki wa majengo na vyombo vya usafiri na usafirishaji, wafanyabiashara na wananchi wote kuhakikisha wananunua au kufanyia matengenezo (service) vifaa na mifumo ya kinga na tahadhari dhidi ya moto kwa Mawakala waliosajiliwa kuuza vifaa vya Zimamoto (Fire Dealers) kwa mujibu wa sheria ya Jeshi.
Imetolewa na;
Ofisi ya Habari na Elimu kwa Umma
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
03 Januari, 2018