Ndugu waandishi wa habari, awali ya yote napenda kumshukuru mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na uhai tulionao kuanzia tulipoanza mwaka 2017 hadi sasa tunapokwenda kumaliza tukiwa salama.
Kadhalika pia napenda kutumia nafasi hii kuvishukuru vyombo vyote vya habari kwa kuonyesha ushirikiano mzuri kwangu ikiwa ni pamoja na kuripoti vizuri habari za jiji la Dar es Salaam, kwani mmekuwa na mchango mkubwa katika kuhabarisha wananchi mambo mbalimbali ninayoyafanya katika jiji hili.
Katika kipindi chote cha mwaka 2017 , mmeonyesha ushirikiano mkubwa kwangu ikiwa ni pamoja na kuripoti habari kwa weledi mkubwa licha ya changamoto mlizokuwa nazo lakini mmefanya kazi yenu na zimeonekana, hivyo sina budi kuwashukuru sana hakika nimeona nakutambua mchango wenu.
pamoja na changamoto zilizopo, napenda kurudia tena natoa shukrani zangu za dhati kwenu kwa kazi zuri ambazo mnazifanya za kuhabarisha Umma wa watanzania.
Aidha napenda kusisitiza kuwa vyombo vya habari msichoke kufanya kazi na jiji la Dar es Salaam badala yake tuendelee kushirikiana katika kuhabarisha Umma mambo ya maendeleo ambayo tunafanya ikiwa ni katika kuhakikisha kuwa ninaleta maendeleo makubwa kwa kipindi ambacho nipo madarakani.
Ndugu waandishi wa habari. Kila ifikapo Desemba 25, kila mwaka wakristo wote nchini wanaungana na wakristo wenzao duniani kusherehekea sikukuu ya krismasi na mwaka mpya.
Katika kipindi hiki cha sikukuu, kumekuwa na utamaduni wa kujitokeza kwa mambo mbalimbali ambayo sio mazuri hususani katika suala zima la usalama , hivyo niwaombe wananchi wote wa jiji la Dar es Salaam kuwa wangaalifu kwa kipindi hiki ili kila mmoja aweze kumaliza mwaka 2017 na tuweze kuuona mwaka 2018 tukiwa salama.
Wazazi natambua kuwa mnawapenda sana watoto wenu, hivyo mkawe wangaalifu kwao ili kuwaepusha na ajali za barabarani, ufukweni, sambamba na kumbi za starehe kwani sio jambo jema kuwahusisha watoto kwenye makundi hayo. Lakini pia niombe wananchi wote , mtulie majumbani na familia zenu mkisherehekea kwa amani.
Ndugu wandishi wa habari. Wapo ndugu zetu ambao wanatoka katika jiji la Dar es Salaam wanasafiri kwenda mikoani kujumuika na familia zao katika kipindi hiki cha sikukuu, nitumie fursa hii kuwaeleza madereva wote wawe makini barabarani ili kujiepusha na ajali zisizo kuwa za lazima.
Aidha napenda kutumia fursa hii kuwaeleza wanachi wa jiji la Dar es Salaam kuwa tutumie muda mwingi katika kufanya mambo ya maendeleo na kuachana na mambo ya kufuatilia siasa ambazo hazina tija.
Hivyo niwaombe sana fanyeni kazi kwa ajili ya manufaa ya maendeleo, mkishirikiana na viongozi wetu ambao mmewachagua kwa kura zenu, kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata, Jimbo, Halmashauri , Jiji pamoja na ngazi nyingine za kitaifa katika Nchi hii.
Mwisho nipende kuwashukuru wananchi wa jiji la Dar es Salaam kwa ushirikiano wenu ambao mnaendelea kuuonyesha kwa Meya wenu, niseme kwamba nipo kwa ajili ya kuleta maendeleo na sio kupambana na mambo ya kisiasa.
Imetolewa leo Desemba 20. 2017
Na Christina Mwagala, Ofisa Habari Ofisi ya Meya wa Jiji