Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma.
Dec 14, 2017
Na Msemaji Mkuu

Huduma Zinazotolewa na Hospitali ya Rufaa ya Taaluma na Tiba (Mamc) Iliyoko Mloganzila

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayo furaha kuwatangazia wananchi wote na wadau wote wa Sekta ya Afya kuwa, Hospitali ya Rufaa ya Taaluma na Tiba (MAMC) ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) iliyoko Mloganzila, jijini Dar es Salaam, imeanza kupokea wagonjwa waliopewa rufaa kwa ajili ya matibabu ya magonjwa ya ndani (internal medicine).

Hii inafuatia kufunguliwa rasmi kwa Hospitali hiyo na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mnamo tarehe 25 Novemba, 2017.

Wizara inapenda kutumia fursa hii kuwafahamisha Waganga Wakuu wa Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda kwamba maelekezo yamekwisha tolewa ya namna ya kuelekeza rufaa za wagonjwa wao katika hospitali ya MAMC.

Aidha, Wizara inapenda kuwataarifu Wananchi na Wadau wa Huduma za Afya kuwa, MAMC ni Hospitali ya kisasa kabisa, na ina uwezo wa kutoa huduma za kibingwa kwa kiwango kama kile ambacho kinatolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Vilevile, MAMC inashirikiana na wataalamu mabingwa kutoka MNH katika kuhudumia wagonjwa.

Taarifa hii ni muhimu kwa kuwa, kumekuwa na uvumi kutoka kwa baadhi ya wadau wanaodhani kuwa hospitali hii ni ya mafunzo, na hivyo haiwezi kutoa matibabu sawa na MNH. Wizara inawahakikishia wananchi na wadau wote kuwa, huduma zinazotolewa na MAMC zinajumisha pia huduma za daraja la ubingwa wa ngazi ya juu  (super specialized services) na zenye ubora stahiki.

Wizara inatoa wito kwa wananchi na wadau wote kupokea na kutumia huduma zinazotolewa na MAMC.

Wizara itaendelea kutoa taarifa za huduma mpya za MAMC kwa kadri zitakavyokuwa zinaanzishwa ili rufaa husika zielekezwe huko.

Dkt. Mpoki M. Ulisubisya.

KATIBU MKUU (AFYA)

14/12/2017

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi