THBUB Yampongeza Rais kwa Kuwafutia Watu 61 Adhabu ya Kifo
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Bahame Tom Nyanduga kwa niaba ya Tume na Wafanyakazi wote wa THBUB anachukua fursa hii kumpongeza kwa dhati Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kufuta adhabu ya kifo kwa watu 61 waliokuwa magereza mbalimbali nchini, wakisubiri utekelezaji wa adhabu ya kifo dhidi yao.
Tume inampongeza sana Mhe. Rais kwa uamuzi wake huo kwani unaendana na Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Na. 62/149 la tarehe 18 Desemba 2007 linalozitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kufuta au kusimamisha utekelezaji wa adhabu ya kifo na kuweka adhabu mbadala.
Tume inatambua kwamba, kama alivyosema Mhe. Rais, msamaha huu haufuti adhabu ya kifo katika sheria za nchini.
Hivyo, kutokana na mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 130(1) (g), Tume inapenda kuchukua nafasi hii kuishauri Serikali kuona uwezekano wa kufuta adhabu ya kifo na kuweka adhabu mbadala, ili iendane na Azimio la Umoja wa Mataifa lililotajwa hapo juu.
Pia, Tume inaisihi Serikali, hususan Idara yake ya Ustawi wa Jamii kuwasaidia, na Wananchi kwa ujumla kuwapokea, wale wote waliopewa msamaha ili waweza kuendelea na maisha yao kama raia wema katika jamii.
Imetolewa na:
Mhe. Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Desemba 9, 2017