Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma
Jan 27, 2021
Na Msemaji Mkuu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane itakuja na ubunifu wa kutatua changamoto katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha sekta hiyo inatengewa fedha za kutosha.

Ameyasema hayo leo katika Kikao na Wadau wa Elimu, Kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni Jijini Zanzibar, ukiwa na madhumuni ya kutafuta ufumbuzi juu ya matatizo yanayoikabili sekta ya elimu.

Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba sekta ya elimu ni lazima ipewe kipaumbele maalum ili kuhakikisha malengo yake yaliyoyaweka yanafanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi kwa kuwekewa fedha.

Alisema kuwa ametaka kwa makusudi kukutana na Wadau ili kuwasikiliza  na hatimae kuangalia hatua gani muhimu zinaweza kuchukuliwa katika kuinusuru sekta ya elimu.

Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kuwepo kwa Mfuko wa kuendeshea sekta ya elimu na kusisitiza kwamba ni vigumu kuiendesha sekta ya elimu bila ya kuwepo kwa fedha.

Alitumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Elimu kukaa na Wadau mmoja mmoja akiwa na maana ya Taasisi ama sekta za elimu ili kujua changamoto walizonazo kabya ya yeye kukutana nao.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa umefika wakati kupitiwa upya kwa Sera ya Elimu ikiwa ni pamoja na kuangalia suala zima la mitaala na kueleza haja ya kukaa pamoja kati ya wadau na Serikali na hatimae kuleta ufumbuzi na serikali iko tayari kufanya hivyo.

Alieleza kwamba suala la masomo mengi kwa wanafunzi wa darasa la kwanza, wanafunzi kuishia darasa la sita badala la saba ni vyema likaangaliwa kama suala hilo lina tija ama lina matatizo kwa lengo la kulipatia ufumbuzi.

Aliongeza kuwa Sheria ya Elimu ya Juu, inaonesha wazi kwamba imepitwa na wakati hivyo, ni vyema taratibu zikachukuliwa katika kulifanyia kazi suala hilo kwani uwepo wa Sera na Sheria inayokwenda na wakati ni jambo muhimu katika sekta ya elimu.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba miundombinu ya elimu ikiwemo madarasa bado ina changamoto hivyo, ni vyema suala hilo likafanyiwa kazi na kueleza kwamba kama itakubalika kipaumbele cha serikali iwe elimu basi bajeti ya serikali na mikopo ya serikali itaelekezwa huko.

Kuhusu vifaa vya kusomea, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba kuna haja ya kuwepo kwa vifaa hasa katika skuli za Msingi na Sekondari na kueleza haja ya kujipanga katika kuhakikisha hilo linafanyiwa kazi.

Alisisitiza haja ya kufanya tathmini ya wafanyakazi katika Wizara ya Elimu ili kuona kwamba vipi wanafanyakazi kwa idadi yao waliopo hasa kwa upande wa walimu.

Alisema kuwa suala la wafanyakazi na maslahi ni jambo kubwa sana kwani mwalimu hawezi kwua na morali ya kufundisha iwapo maslahi yake hayako vizuri.

Rais Dk. Mwinyi alitoa wito kwa viongozi aliowateua kuhakikisha wafanyakazi wanapata maslahi yao bila ya kuwepo lugha za kijeli kwa wafanyakazi hao.

Alieleza haja kwa kila mfanyakazi kuwajibika katika eneo lake na kueleza kwamba kwa wale wasiowajibika wajue kwamba hawatendi haki.

Katika hotuba yake hiyo, Dk. Mwinyi alieleza umuhimu wa ushirikishwaji kwa skuli binafsi huku akieleza kwamba  Serikali itaangalia suala zima la mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutokana na changamoto zilizopo.

Alieleza haja ya kufanywa kwa tathmini juu ya suala zima la ugatuzi kwani inaonesha kwamba wengi wa wafanyakazi waliotoa maoni yao katika kikao hicho wameeleza kwamba bado zoezi hilo halijasaidia sana.

Aidha, alisisitiza haja ya kufanywa kwa tathmini juu ya kuunganishwa kwa vyuo vikuuna vile vyuo vidogo kwani waliofanya uwamuzi huo pia, nao walikuwa na hoja hivyo ni vyema kukangaliwa kama kuna mafanikio ama hasara.

Alisema kuwa tayari ameshafanya mazungumzo na Jaji Mkuu juu ya kuwepo kwa Mahakama maalum ya Udhalilishaji na kusema kwamba jambo hilo ni lazima lipigwe vita kwa mashirikiano ya pamoja.

Alieleza haja ya kuwasaidia walimu wanaowasomesha wanafunzi wenye mahitaji maalum na kupokea ombi lao la kupatiwa vifaa maalum vya kusomeshea “software” huku akieleza umuhimu wa kuimarisha elimu ya amali.

Kwa upande wa vyuo vya Qur-an, aliitaka Ofisi ya Mufti ikae pamoja na Wizara ya elimu kuangalia suala zima la uendelezaji wa masomo katika madrsa na kusisitiza kwamba kwa hali ilivyo Zanzibar somo la dini linaumhimu mkubwa.

Pia, alieleza haja ya kuongeza nguvu baina ya wadau na Serikali kwa kuwasaidia vijana waliokuwa hawakubahatika kuendelea na masomo ya Sekondari na kutoa pongezi kwa wadau wote wanaowasaidia vijana hao.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja kwa vikao hivyo kuwa na tija huku akitoa shukurani kwa wadau kwa kuwa tayari kufanya kazi na serikali katika kuimarisha sekta ya elimu huku akiahidi kwamba tatizo lililokuwepo katika Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) atalifanyia kazi.

Nao wadau katika michango yao walieleza haja ya kuimarishwa kwa Sera ya Elimu, utendaji kwa Vituo vya Walimu na kuomba Idara ya Ukaguzi iwe chini ya Ofisi ya Rais ama Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais badala ya kuwepo katika Wizara ya Elimu.

Wadau hao walieleza changamoto zilizopo katika maslahi ya walimu, udhalilishaji kwa wanafunzi, mfomo usio rasmi wa usomeshaji, umhimu wa kusomeshwa kwa somo la Dini  ya Kiislamu, ushirikishwaji wa skuli binafsi katika maamuzi sambamba na changamoto waliyonayo katika mfumo mzima wa ugatuzi.

Mapema, Rais Dk. Mwinyi alijumuika pamoja na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na serikali ndugu, jamaa na marafiki kumsalia na kumuombea dua Marehemu Abbas Khalil Mirza huko katika Msikiti wa Shia Jamati, Kiponda Jijini Zanzibar.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi