RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na Zanzibar katika kutokomeza maradhi ya kichocho.
Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China aliepo Zanzibar Xie Xiaowu pamoja na ujumbe wa (WHO) ukiongozwa na Dk. Dirk Engels wakiwa na madaktari wanaosimamia mradi wa majaribio wa kichocho uliofanyika kisiwani Pemba.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alieleza kuwa China imeanza kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya afya mara tu baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964, hivyo hatua zake za kushirikiana na (WHO) katika mradi huo ni uendelezaji wa mashirikiano hayo ya kihistoria.
Rais Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina uhusiano na ushirikiano mwema na Serikali ya Watu wa China pamoja na Shirika hilo la Afya Ulimwenguni (WHO) kwa miaka mingi hivyo kuanza kwa mradi huo ambao utakuja na matokeo mazuri ni uthibitisho wa mashirikiano hayo.
Akielezea jinsi Serikali ya Watu wa China ilivyoiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya afya, Rais Dk. Shein alisema nchi hiyo imesaidia ujenzi wa Hospitali ya Mkoani Pemba, kuleta timu ya madaktari, vifaa tiba pamoja na mambo mengineyo yenye mnasaba na maendeleo ya sekta ya afya.
Alieleza kuwa mafanikio hayo yote yamekuja baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Xi Jinping wakati alipoitembelea Tanzania na pale Dk. Shein alipopata fursa ya kuitembelea nchi hiyo ambapo Rais Xi aliahidi kuyafanya yale yote aliyoyatakeleza ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Mkoani.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza jinsi alivyofurahishwa na zoezi hilo la majaribio ya pamoja katika kupambana na maradhi hayo lililofanywa kati ya madaktari wataalamu
kutoka nchini China kwa kushirikiana na (WHO).
Dk. Shein alieleza kuwa matokeo ya majaribio hayo ya maradhi ya kichocho ambayo tokea yameanza hadi hivi sasa yamepungua mpaka kufikia asilimia moja 1% ni matokeo yanayotia moyo katika kupambana na maradhi hayo hasa kisiwani Pemba ambako majaribio hayo yamefanyika.
Alisisitiza kuwa Zanzibar ina historia kubwa ya mashirikiano kati yake na (WHO) katika kupambana na maradhi kadhaa ambapo miongoni mwa maradhi hayo ni Malaria ambapo Zanzibar imeweza kuyatokomeza na kuwa mfano duniani.
Nae Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China aliepo Zanzibar Xie Xiaowu alieleza kuwa China na (WHO) zimedhamiria kwa makusudi kuiunga mkono Zanzibar katika kupambana na maradhi ya kichocho.
Alisema kuwa anamatumaini makubwa kuwa matokeo ya majaribio hayo yatakuwa mazuri na yataweza kusaidia azma ya pamoja iliyokusudiwa ya kuwasaidia wananchi wa Zanzibar katika kupambana na maradhi hayo.
Alieleza kuwa Serikali ya China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya pamoja na sekta nyenginezo za maendeleo kwani nchi hizo zina historia kubwa katika uhusiano na ushirikiano wake uliopo.
Mapema Dk. Dirk Engels kutoka Shirika la (WHO) alimueleza Dk. Shein kuwa majaribio hayo ni mpango wa pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Alieleza kuwa Zanzibar imeteuliwa kuwa ni sehemu ya majaribio ya mradi huo wa mapambano ya maradhi ya kichocho hasa kisiwa cha Pemba kutokana na vigezo kadhaa vilivyopo ambayo vinaonesha matokea chanya huku akieleza azma ya kuendeleza mradi huo katika baadhi ya maeneo ya Zanzibar.
Mkuu wa mradi huo Yang Kun kutoka taasisi ya “Jiangsu Institute of Parasitic Diseases”nchini China alisema kuwa mradi huo ni wa muda wa miaka miwili ambao umeonesha mafanikio makubwa kutokana na mashirikiano waliyoyapata kutoka kwa wananchi wa kisiwani Pemba pamoja na viongozi wao.