Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 04 Januari, 2019 ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa mauziano ya mahindi kati ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Shirika la Chakula Duniani (WFP) uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mkataba huo umetiwa saini na Kaimu Mtendaji Mkuu wa NFRA Bi. Vumilia Zikankuba na Mwakilishi na Mkurugenzi Mkazi wa WFP hapa nchini Bw. Michael Danford, ambapo WFP itanunua tani 36,000 zenye thamani ya shilingi Bilioni 21 kutoka NFRA.
Baada ya kutia saini mkataba huo Bw. Michael Danford amesema mahindi hayo ni sehemu ya tani 160,000 za chakula zenye thamani ya shilingi Bilioni 132.2 zilizonunuliwa na WFP nchini Tanzania katika mwaka 2018, ikiwa ni ongezeko la kutoka shilingi Bilioni 63.6 zilizotumika kununua chakula katika mwaka 2017.
Bw. Michael Danford amebainisha kuwa kutokana na uhusiano mzuri wa Tanzania na WFP uliodumu kwa miaka 40 sasa, mwaka 2017 shirika hilo liliweka mpango mkakati unaoendana na Mpango wa Maendeleo wa Tanzania, ambapo limeamua kuwa mnunuzi mkubwa wa mazao ya chakula nchini Tanzania kwa ajili ya kusaidia wakimbizi na nchi jirani zenye matatizo ya chakula na kwamba WFP inatarajia kuendelea kuongeza kiwango cha chakula kitakachokuwa kikinunuliwa kutoka Tanzania.
Ameahidi kuwa WFP itaendelea kufanya kazi kwa karibu na NFRA na taasisi zingine zinazohusika katika ununuzi wa chakula ikiwemo Shirika la Reli Tanzania (TRC) ambako imetoa msaada wa shilingi Bilioni 1.4 za kukarabati mabehewa 40 ya treni ili kurahisishausafirishaji wa mazao.
Pamoja na kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali zikiwemo Jeshi la Polisi, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kuhakikishia wanaondoa urasimu na kuharakisha ununuzi wa mazao yanayonunuliwa na WFP (ikiwemo tani hizo 36,000 za mahindi) ili wakulima wa Tanzania wanufaike na fursa hiyo.
Mhe. Rais Magufuli ameipongeza WFP kwa uamuzi wake wa kununua chakula kutoka Tanzania kwa ajili ya kusaidia wakimbizi na nchi zenye matatizo ya chakula na ameitaka NFRA kutoa tani zote 45,000 za mahindi ambazo WFP waliomba kununua, ili fedha zitakazopatikana zitumike kununua mahindi mengine kutoka kwa wakulima.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameitaka NFRA kujipanga vizuri katika shughuli zake ili kuondokana na utaratibu wa kuwa inapatiwa fedha kutoka Serikalini kila mwaka kwa ajili ya kununua mazao ya hifadhi ya chakula, ilihali mazao yaliyopo hifadhini yakiuzwa kiujanjaujanja kwa wafanyabiashara tena kwa bei ya kutupa.
“Nyinyi NFRA wapeni hawa WFP tani zote 45,000 wanazozihitaji, na hata wakihitaji tani 100,000 wapeni au hata 200,000 wapeni, mkipata hizo fedha nendeni mkanunue mazao ya wakulima wanaohangaika na soko. Lakini pia punguzeni matumizi makubwa ya fedha za kugharamia zoezi la ununuzi wa mazao” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Pia Mhe. Rais Magufuli amewataka wafanyabiashara kuacha kulalamika na badala yake wafanye biashara zao kwa uwazi na kwamba Serikali itawaunga mkono.
Mapema Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Innocent Bashungwa amesema wizara imechukua hatua kadhaa za kuimarisha mazingira kwa WFP kununua mahindi na mazao mengine hapa nchini, na kwamba jambo hilo linafanywa sambamba na mkakati wa kufungamanisha kilimo na viwanda na kuimarisha ushirika ili kupanua zaidi uwigo wa soko la mazao ya wakulima.
Hafla ya utiaji saini mkataba huo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba, Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias Kwandikwa, Makatibu Wakuu, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na wakuu wa taasisi mbalimbali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Januari, 2019