RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kwamba maonyesho ya Utalii yanayofanyika Zanzibar ni muhimu kwa Serikali na wananchi kwa kuwa yamelenga kuitangaza Zanzibar na sekta ya utalii ambayo ndio muhimili mkuu wa uchumi.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika viwanja vya hoteli ya Verde, Mtoni Mjini Zanzibar katika ufunguzi wa maonyesho ya Utalii Zanzibar ya mwaka 2018 ambayo yalihudhuriwa na viongozi mbali mbali wakiwemo Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Makamo wa Pili wa rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, wadau wa utalii na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali pamoja na wananchi.
Katika maelezo hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa Utalii umekuwa ukichangia asilimia 27 kwa Pato la Taifa na asilimia 80 ya fedha za kigeni zinazokusanywa ambapo muda wanaokaa watalii nchini umeongezeka ambapo hivi sasa mtalii hutumia wastani wa siku 8 badala ya 6 kama ilivyokuwa miaka 5 iliyopita.
Alifahamisha kwamba takwimu hizo ni njema kwa Serikali, wanchi, wawekezaji na wadau wote katika sekta ya utalii kwa kuwa zinabainisha kwamba sekta ya utalii imekuwa ikikuwa kwa kasi na watalii wanapenda kubakia nchini huku wakiwa tayari kutumia fedha wanazokuja nazo kufurahishwa na ukarimu wa watu wa Zanzibar.
Rais Dk. Shein alieleza juhudi mbali mbali za kuimarisha utalii zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali zikiwemo kuanzisha mpango wa “Utalii kwa wote” ambapo lengo kuu la mpango huo ni kuhakikisha kwamba sekta ya utalii inawanufaisha wananchi wote wa Zanzibar na kuimarisha ustawi wa wananchi kwa jumla.
Alisisitiza kuwa juhudi mbali mbali zinaendelea kuchukuliwa na Serikali za kuendeleza sekta ya utalii zinaenda sambamba na mikakati na malengo ya MKUZA, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs).
Alieleza imani yake kwamba maonyesho hayo ni njia bora na madhubuti ya kuitangaza Zanzibar pamoja na fursa mbali mbali zilizopo za kiuchumi kwa wawekezaji ambapo pia, washiriki watazifahamu fursa zilizopo nchini na haja ya washiriki hao kuzichangamkia.
Alisema kuwa Zanzibar imejaaliwa na mazingira yanayovutia na ina vivutio vingi vya utalii zikiwemo fukwe na sehemu za historia pamoja na hoteli nyingi za kisasa ikiwemo Hoteli hiyo ya Verde.
Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza juhudi kubwa zilizochukuliwa na Serikali katika kuimarisha miundombinu ya barabara kwa kuzijenga upya na kuzifikisha katika maeneo muhimu ya utalii kwa lengo la kuimarisha sekta hiyo sambamba na shughuli za uwekezaji na huduma kwa wananchi.
Alieleza historia ya Zanzibar kwa kubainisha kwamba Zanzibar ilikuwa ni kituo kikuu cha Biashara katika Afrika ambacho kilikuwa kikiwavutia wafanyabiashara na wavumbuzi kutoka Mataifa mbalimali ya Ulaya, Asia na Mashariki ya Kati na Mashariki ya mbali.
Aidha, Rais Dk. Shein aliiagiza Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kuhakikisha kuwa watu wanaotembeza wageni wawe wamepatiwa mafunzo yanaayostahiki, wawe na vibali na wahakikiwe kila baada ya muda ili kuhakikisha kwamba hawaharibu historia ya Zanzibar kwa kuisimulia isivyo au kwa kuzingatia matakwa na utashi wao binafsi.
Dk. Shein alieleza juu ya dhamira ya Serikali ya kuifikisha Zanzibar katika kiwango cha nchi zenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020 na kubainisha kwamba hivi sasa wawekezaji wengi wamekuwa wakija nchini kutokana na kuziamini Sera pamoja na mazingira mazuri yalioandaliwa na Serikali.
Alieleza kuvutiwa na maudhui ya maonyesho hayo isemayo “Responsible Tourism for a Better and Greener Tomorrow”,akiwa na maana kwua Utalii anaotilia mkazo uhifadhi wa mazingira kwa lengo la kuleta mustakbali mwema kwa maisha ya baadae.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza juhudi zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kukuza hali ya usalama ndani ya mji Mkongwe wa Zanzibar ambao ndio mafanikio maarufu ya utalii na urithi wa kimataifa kama ulivyotambuliwa na UNESCO.
Akieleza juu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa ufungaji wa kamera katika Mji Mkongwe wa Zanzibar uliofanywa na Serikali aliouzindua tarehe 04 Oktoba, 2018 na kufahamisha hivi sasa Mji wa Zanzibar na maeneo yake yako katika usalama zaidi kwa wakaazi wake wawekezaji na watalii.
Kadhalika alifahamisha kwamba katika malengo na juhudi za Serikali katika utekelezaji wa mradi wa Huduma za Mji (ZUSP) ambao pamoja na mambo mengine umelenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za mji pamoja na kuyatunza majengo ya urithi wa utamaduni na mazingira ya asili ya Mji Mkongwe.
Rais Dk. Shein alieleza azma ya Serikali kulifukia eneo la babari la Gulioni kama alivyofanya mfanya biashara maarufu Said Baghresa la kufukia bahari katika eneo la Hoteli ya Verde sambamba na ujenzi wa miji ya kisasa katika eneo la Kwahani na Chumbuni na kueleza kuwa Zanzibar itabadilika sio muda mrefu na kusisitiza falsafa yake ya kutofanya kazi kwa mazoea kuwa ni vyema ikachukua mkondo wake.
Katika hafla hiyo, Rais Dk. Shein alitoa vyeti maalum kwa wadau mbali mbali waliosaidia kuuimarisha na kuutangaza utalii wa Zanzibar ndani na nje ya nchi kwa kutumia huduma wanazoziendesha yakiwemo makampuni mbali mbali, hoteli, Jumuiya na Taasisi za umma na binafsi.
Mapema Rais Dk. Shen alitembelea mabanda maalum ya maonyesho yaliyozishirikisha Kampuni mbali mbali za kitalii, taasisi binafsi na za umma, Kampuni zinazotoa huduma za kitalii, Jumuiya pamoja na Hoteli za Kitalii.
Nae Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shen kwa juhudi zake za kuimarisha sekta ya Utalii ikiwa ni miongoni mwa utekelezaji wake wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015-2020.
Waziri Kombo alieleza kuwa Wizara yake imo katika hatua za kuhakikisha inavuka lengo la kufikia watalii nusu milioni kwa mwaka na kueleza kuwa lengo hilo litavukwa kwani alithibitisha kuwa hadi Julai mwaka huu walifikia watalii 263,000 ambapo wakiendelea na hatua hiyo hadi mwisho wa mwaka huu watafikia watalii 520,000.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale Khadija Bakari Juma alieleza hatua zilizochukuliwa na Wizara pamoja na wadau wengine wa utalii na wafadhili wengine katika kufanikisha maonyesho hayo yenye lengo la kuimarisha sekta ya utalii nchini.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk