Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma
Aug 17, 2018
Na Msemaji Mkuu

 

MA’DC FANYENI TATHMINI YA MALI ZA HALMASHAURI-MAJALIWA 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa wilaya nchini washirikiane na Madiwani katika halmashauri zao wafanye tathmini ya mali zote zinazomilikwa na halmashauri vikiwemo vibanda vya biashara ili kujiridhisha kama viwango vinavyotozwa vinalingana na hali halisi ya uchumi kwa sasa.

Amesema licha ya tathmini hiyo kuwawezesha kufahamu viwango vinavyotozwa, pia itasaidia halmashauri kubaini watu wa kati ambao wanawatoza wafanyabiashara fedha nyingi na kuilipa halmashauri fedha kiduchu, jambo linalochangia kuikosesha Serikali mapato inayostahili.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Agosti 17, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya Mji wa Nzega na wa Halmashauri ya wilaya ya Nzega pamoja na Madiwani katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Nzega akiwa kwenye ziara yake ya kikazi wilayani Nzega, Tabora.

Ametoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Nzega Mjini, Husein Bashe kuomba Serikali iingilie kati mgogoro uliopo baina ya halmashauri na wafanyabiashara kuhusu mradi wa vibanda vya biashara katika eneo la Soko Kuu la Nzega ambavyo vimejengwa na wafanyabiashara katika ardhi ya halmashauri kwa makubaliano ya kulipa kodi.

Uongozi wa halmashauri ya Mji wa Nzega uliamua kupitia upya mkataba wa mradi huo kwa sababu ulikuwa hauinufaishi, hivyo ilianzisha mpango wa maboresho ambapo ilibaini kuwepo kwa watu wa kati waliokuwa wakiwatoza wafanyabiashara zaidi ya sh 150,000 kwa mwenzi na kuilipa halmashauri sh. 30,000 kwa mwezi.

Pia ilibaini kwamba baadhi ya wamiliki wa awali wa vibanda waliviuza kwa wafanyabiashara wengine kwa bei kubwa bila ya kuishirikisha halmashauri na ilivyotaka kuvichukua ili wafanyabiashara waendelee kuwa wapangaji kwa lengo la kuondoa mtu wa kati, ndipo ulipoibuka mgogoro wa umiliki wa vibanda hivyo

Waziri Mkuu amesema migogoro ya aina hiyo huwa haiishi kwa wakati katika maeneo mengi kwa sababu baadhi ya vibanda hivyo vinamilikiwa na Wakuu wa Idara, Madiwani na baadhi ya watumishi katika hailashauri husika, jambo linalozikosesha halmashauri mapato. “Wakuu wa wilaya shughulikieni hili,”.

Pia, Waziri Mkuu amezishauri halmashauri zinazomiliki vibanda vya biashara hususani kwenye maeneo yenye migogoro watumie leseni za biasahara zinazofanyakazi kwa kuzitambua na kuingia mikataba na wamiliki wake ili kuondoa uwepo wa mtu wa kati.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wanaomiliki vinanda vya biashara kwenye eneo hilo watoe taarifa za umiliki wao ili kuondoa mgongano wa kimaslahi pindi wanapokuwa kwenye vikao vya kujadili namna bora ya kuipatia ufumbuzi migogoro ya vibanda vya biashara vinavyomilikiwa na halmashauri katika maeneo yao.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa halmashauri na wilaya wawahamasishe wananchi kwenye maeneo yao juu ya umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), hivyo watakuwa wamejihakikishia upatikanaji wa huduma za afya bure kwao na familia zao.

Pia amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bw. Agrey Mwanri kwa jitihada kubwa za kupanua wigo wa kuboresha huduma za afya kupitia CHF, ambapo kwa mkoa huo wanachama wa mfuko huo wanaweza kutibiwa kwenye hospitali zote za Serikali tofauti na maeneo mengine ambayo huduma hiyo inaishia kwenye hospitali za wilaya tu.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

IJUMAA, AGOSTI 17, 2018.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi