Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Atupele Mwakibete, ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kushirikiana kwa karibu na taasisi zote za Serikali na zisizo za Serikali zinazotoa huduma katika viwanja vya ndege ili kuboresha utoaji wa huduma viwanjani.
Amesema hayo jijini Dar es Salaam mara baada ya kukagua jengo la tatu la abiria katika kiwanja cha ndege cha Kiimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), na kusisitiza ushirikiano utaboresha huduma na kuongeza mapato.
"Viwanja vya ndege vya Julius Nyerere (JNIA), KIA, Mbeya, Mwanza, Dodoma na Arusha ambavyo kwa sasa vina idadi kubwa ya abiria wanaoingia na kutoka endeleeni kuongeza ubunifu", amesema Mhe. Mwakibete.
Naibu Waziri huyo amesema uimarishaji wa utoaji wa huduma viwanjani unategemea ushirikiano wa karibu wa wadau ambao utaongeza imani ya mashirika mbalimbali ya ndege ndani na nje ya nchi na hatimaye kuongeza mapato.
“Niwapongeze kwa usimamizi mzuri wa viwanja vya ndege nchini na niwaagize kuwa lazima mfanye vikao vya mara kwa mara na wadau wanaofanya kazi katika viwanja hivi, ili kupunguza malalamiko na kulaumiana hasa zinapotokea changamoto za usafirishaji wa nyara za Serikali”, amesisitiza Naibu Waziri Atupele.
Naibu Waziri Mwakibete ameitaka TAA kuandaa mikakati inayotekelezeka ya kuvifanya viwanja vingine vya mikoani kujiendesha vyenyewe badala ya kutegemea fedha zinazopatikana katika Kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere cha Dar es Salaam.
“Tuna viwanja zaidi ya 50, lakini sehemu kubwa ya viwanja hivyo vinaitegemea kifedha kiwanja cha JNIA na sasa haiwezekani, jipangeni mje na mikakati thabiti ya kuhakikisha viwanja vikubwa vya mikoa vinajitegemea na kujiendesha", amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.
Kwa upande Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Hamis Amiri amesema kwa sasa Mamlaka inaendelea na utekelezaji miradi mikubwa ya ujenzi wa viwanja ikiwemo kiwanja cha ndege cha Msalato mkoani Dodoma ambapo ndio makao makuu ya nchi.
Naye Meneja wa Jengo la Tatu la Abiria JNIA, Mhandisi Barton Komba ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya Viwanja na kumuahidi Naibu Waziri kuwa Mamlaka itaendelea kuzingatia viwango vya usimamizi kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO).
Naibu Waziri Atupele yuko mkoani Dar es Salaam kwa ajili ya kutembelea, kufahamiana na kuzungumza na viongozi na watumishi waliopo katika taasisi za Sekta ya Uchukuzi na pamoja na kukagua miradi ya kisekta.