Switzeland imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kusaidia Sekta mbalimbali za Maendeleo hasa katika suala la Afya, kuongeza ajira na kukuza ujuzi .
Hayo yamebainishwa wakati wa Mkutano Jijini Dodoma kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Philip Isdor Mpango na Balozi wa Switzerland hapa nchini Bi. Florence Tinguely Mattli, ulioangazia uhusiano kati ya nchi hizo mbili na namna ya kuboresha ushirikiano.
Katika Mkutano huo Waziri Mpango amemuomba Balozi huyo kuangalia uwezekano wa kuwapa mafunzo madaktari Bingwa nchini ili kukidhi uhitaji uliopo hasa katika Jiji la Dodoma ambalo ndio makao Makuu ya Nchi na idadi ya wakazi wake inaongezeka, na pia kufadhili mafunzo kwa Watumishi wa umma ili kuwajengea uwezo katika kada mbalimbali lengo likiwa ni kuongeza ufanisi wa kazi.
Aidha waziri Mpango aliongeza kuwa miundombinu ya Jiji la Dodoma inahitaji kuboreshwa hivyo Switzerland iangalie uwezekano wa kufadhili miradi ya maendeleo katika Sekta ya Maji na mazingira.
“Tanzania ni nchi ya tatu kwa kuwa na mifugo mingi Barani Afrika lakini ufugaji wa mifugo hiyo hauna ubora, kwa kuwa Switzerland imeendelea katika Sekta ya Mifugo fursa ipo ya uwekezaji katika eneo hilo hapa nchini” alieleza Dkt. Mpango.
Amesema kuwa Serikali ya Tanzania inafanya jitihada mbalimbalimbali kukabiliana na umasikini hivyo ni vema Washirika wa Maendeleo wakatambua kuwa hatua mbalimbali ambazo Serikali inazichukua kama kupambana na wakwepa kodi na kuboresha mikataba zina lengo la kuboresha maisha ya watanzania kwa kuhakikisha wananufaika na rasilimali nyingi zilizopo nchini na wawekezaji waweze kunufaika pia.
Waziri Mpango amesema kuwa Switzerland inashiriki kikamilifu katika miradi ya Matumizi bora ya misitu hususani Mkoani Morogoro, kuboresha ujuzi na kukuza ajira kwa Watanzania.
Kwa upande wake Balozi wa Switzerland nchini Bi. Florence Tinguely Mattli, amesema kuwa Uhusiano kati ya Nchi yake na Tanzania umezidi kuimarika na kuahidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika sekta mbalimbali za maendeleo huku akisisitiza suala la kuzingatia uwazi na mazingira bora ya uwekezaji kwa kuwa ni chachu kubwa ya kuvutia uwekezaji wenye tija kwa pande zote mbili.
Dkt. Mpango amemhakikishia Balozi huyo kuwa Serikali inatoa na itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika katika suala la uwekezaji kwa kuwa Tanzania inaongozwa kwa utawala wa sheria unaozingatia haki.
Imetolewa na ;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango