Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imefanya juhudi kubwa kuhakikisha suala la maji ambalo lilikuwa changamoto katika maeneo mengi nchini limefanyiwa kazi kikamilifu.
Rais Samia aliongea hayo leo mkoani Singida wakati akiwaaga na kuwashukuru Wananchi wa Mkoa huo kwa kumpokea na kumkarimu vizuri yeye na ujumbe wake katika kipindi chote cha ziara yake ya kikazi katika mkoa huo na wilaya zake.
Amesema katika ziara hiyo ametembelea maeneo mengi, amekagua kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya elimu, miundombinu, maji na umeme na kwamba amefurahi Mkoa mzima wa Singida hakuna sehemu ambayo amepokelewa na madumu wala ndoo za maji zikiwa tupu.
“Maeneo mengine tulikuwa tukiwekewa maji kwenye chupa, unaletewa pale ulipokaa na unaulizwa kwamba haya ndio maji wananchi tunayokunywa na nyinyi mnakunywa haya? Leo nina faraja kusema kwamba suala la maji tumelifanyia kazi ipasavyo na wananchi kwa kiasi kikubwa wanafaidika na kazi iliyofanywa ya upatikanaji wa maji,” alisema Rais Samia.
Aidha, alisema Wilaya ya Iramba ni sehemu ya Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, ambapo unalenga kufikia vijiji 178 katika Wilaya ya Singida na Wilaya ya Singida Vijijini, Ikungi, Manyoni, Nkalama na Iramba.
“Asilimia 90 ya kazi yote imekamilika, na tunatarajia mwaka kesho katikati ya mwaka Singida yote kama mkoa itakuwa inawaka umeme, tunaendelea kuchukua hatua za muda mfupi na muda mrefu za kuimarisha Gridi ya Taifa ili tuondokane na kero ya umeme kukatika mara kwa mara,” alisema Rais Samia